Na Suzy Luhende, Shinyanga
Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga linamshikilia Grace Godwin(23) Mkazi wa Mtaa wa Sido Kata ya Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga kwa tuhuma za kumchoma moto mikono yote miwili mtoto wake kwa tuhuma za kula wali.
Tukio hilo lilitokea April 27, 2023 katika Mtaa huo wa Sido baada ya mama huyo kumchoma moto mtoto wake mwenye umri wa miaka saba anayesoma darasa la kwanza kwa madai ya kula wali uliobaki (kiporo) bila kuruhusiwa.
Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari wanamshikilia mwanamke huyo kwa hatua zaidi za kisheria na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
“Tunamshikilia mtuhumiwa ambaye anaitwa Grace ni mama mzazi wa mtoto anayedaiwa kuchomwa moto mikono yake yote miwili,tukio hili ni baya na vitendo hivyo vya ukatili tunalaani vikali visijirudie”amesema Kamanda Magomi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Sido Kata ya Ibinzamata Emmanuel Kayange amesema alipata taarifa za tukio hilo na kuamua kufuatilia na kubaini kweli mtoto kachomwa moto na mama yake mzazi kama inavyodaiwa.
Mwenyekiti amesema kutokana na tukio hilo walimuita mama mzazi wa mtoto pamoja na bibi yake Agnes Mgaya na kuwahoji ambapo walibaini mtoto huyo ana siku mbili amechomwa moto wakiendelea kumpa matibabu nyumbani.
Aidha mtoto aliyechomwa moto mikono yote miwili amesema mama yake alimchoma moto kwa kutumia mfuko ambao aliuwasha na kuniwekea mikononi kwa sababu nilikula wali uliokuwa umebaki.
Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Sido wamesema kitendo kilichofanywa na Grace Godwin kumchoma moto mtoto wake kwa madai ya kula chakula ni ukatili mkubwa ambao unapaswa kukemewa vikali ili kukomesha matukio hayo.
Fatuma Ramadhan mkazi wa mtaa huo amesema mtoto aliyefanyiwa ukatili na mama yake mzazi amekuwa akipigwa mara kwa mara na kuiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukubwa wa tatizo kwa kuwahoji mama na bibi wa mtoto huyo.
“Kwa kweli nashindwa kuelewa kwanini watu hawataki kusema ukweli, huyu mtoto anaishi kwa shida anapigwa mno hata ukimuangalia mgongoni na kwenye mikono ana alama za fimbo hili tukio la kuchomwa moto ndilo ambalo limeonekana”, amesema Fatuma.
Shaaban Juma mkazi wa eneo hilo amesema tukio hilo linasikitisha kwani mtoto alikuwa na haki ya kula chakula kwa kuwa hapo ndiyo nyumbani badala ya kuanza kuzunguka mitaani akiomba omba chakula.
Juma amewataka wazazi na walezi kuwa na moyo wa upendo na hofu ya Mungu kwani watu wanaogopa moto, lakini wengine wanachukuwa moto huo na kumchoma binadamu mwenzio ambaye ni mtoto wako jambo ambalo linasikitisha.
Kwa upande wao wadau wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto akiwemo Anascholastika Ndagiwe,amesema mtoto huyo amefanyiwa unyama na mama yake na kuziomba mamlaka husika kuchukuwa hatua kali.
Amesema matukio ni mengi ya ukatili kwa watoto yanafanyika hivyo na serikali inatakiwa kuchukuwa hatua kali kwa watu wanaofanya matukio hayo ili kuyakomesha na kuwawezesha watoto kuishi katika mazingira salama.
Mtoto aliyechomwa moto na mama yake mzazi
Post a Comment