BENKI YA CRDB YAPATA CHETI CHA VIWANGO VYA KIMATAIFA CHA USIMAMIZI WA HUDUMA ZA TEHAMA ISO 20000-1:2018

 


BENKI YA CRDB YAPATA  CHETI
Dar es Salaam 11 Desemba 2023 – Benki ya CRDB leo imekabidhiwa cheti cha viwango vya Usimamizi wa Huduma za TEHAMA cha ISO 20000-1:2018 kilichotolewa na Shirika la Viwango la Uingereza (BSI). Cheti hicho kimekabidhiwa katika hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Benki yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Akipokea cheti hicho kutoka kwa Mkurugenzi Mkaazi, na Mkuu wa Sera za Biashara na Uwekezaji Ubalozi wa Uingereza, Afisa Uendeshaji Mkuu wa Benki ya CRDB amesema cheti hicho ni ishara ya dhamira ya dhati ya Benki ya CRDB katika kuhakikisha mifumo, taratibu, na huduma za TEHAMA za benki hiyo zinakidhi ubora wa kimataifa.

Mwile alisema Benki ya CRDB imekuwa ikiwekeza katika mifumo ya kisasa na hivyo kupelekea mabadiliko makubwa katika huduma zake za TEHAMA kufikia viwango vya kimataifa. Hata hivyo mazingira ya biashara yamekuwa yakibalika kwa kasi kutokana na ukuaji wa teknolijia jambo ambalo limepelekea benki hiyo kufanya mchakato wa kuboresha viwango vyake.

“Tukitambua umuhimu wa kuwa na mifumo ya utoaji huduma iliyo na viwango bora, Benki ilifanya mchakato wa kupata cheti cha ubora wa ISO 20000 cha usimamizi wa huduma. Tulipitia mchakato mrefu uliohusisha uboreshaji wa michakato yetu ya usimamizi wa huduma za TEHAMA,” alisema Mwile.

Mwile aliongezea kuwa benki hiyo pia iliwekeza mipango ya kina ya mafunzo na uhamasishaji ili kuhakikisha wafanyakazi wanaelewa mahitaji ya viwango vya ISO 20000 na kutambua majukumu yao muhimu katika michakato ya usimamizi wa huduma za TEHAMA. Hii ilienda sambamba na kuanzishwa kwa utamaduni wa kuboreha mifumo ya TEHAMA mara kwa mara.

Akielezea faida za kupata uthibitisho wa kiwango hicho cha kimataifa cha ISO 2000, Mwile alisema kunasaidia kuchochea michakato na taratibu zinazohakikisha huduma za TEHAMA zinatolewa kwa ufanisi na kukidhi viwango vya kimataifa, hivyo kutoa uzoefu uliobora kwa wateja.

“ISO 20000 pia inakuza utamaduni wa kuboresha mara kwa mara. Cheti hiki kinatuhimiza kutathmini na kurekebisha mara kwa mara michakato yetu ya usimamizi wa huduma za TEHAMA, kuhakikisha tunaendana na mabadiliko ya mahitaji ya wateja na maendeleo ya teknolojia,” aliongezea.

Akikabidhi cheti hicho Mkurugenzi Mkaazi, na Mkuu wa Sera za Biashara na Uwekezaji Ubalozi wa Uingereza, Anna-Maria Mbwette ameipongeza Benki ya CRDB kwa cheti hicho cha ubora wa kimataifa na kusema kunaonyesha dhamira yake katika ubora, usalama na usimamizi madhubuti.


Anna-Maria alisema kupata ISO 20000 katika huduma za TEHAMA kutasaidia benki hiyo kujenga imani sit u kwa wateja wake, bali pia wawekezaji na washirika wa kimataifa kwani viwango hivyo vinatambulika na kutumika kote duniani.


Kiwango cha ubora wa ISO 2000O katika usimamizi wa huduma za TEHAMA ni mwendelezo wa jitihada za Benki ya CRDB katika kufikia viwango vya kimataifa kwani benki hiyo tayari imepata vyeti vya ubora vya ISO/IEC 27001:2013 cha usimamizi wa usalama wa taarifa, na ISO 22301:2019 cha mipango, mifumo, na michakato ya uendeshaji biashara yenye ufanisi.
Afisa Uendeshaji Mkuu Benki ya CRDB, Bruce Mwile, akipokea Cheti cha Ubora cha Usimamizi wa Huduma za TEHAMA cha ISO 20000-1:2018 kutoka kwa Mkurugenzi Mkaazi, na Mkuu wa Sera za Biashara na Uwekezaji, British High Commission, Anna-Maria Mbwette ambaye amekabidhi kwa niaba ya Shirika la Viwango la Uingereza (BSI) katika hafla fupi iliyofanyika leo 11 Desemba 2023 Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza wakati hafla fupi ya kupokea Cheti cha Ubora cha Usimamizi wa Huduma za TEHAMA cha ISO 20000-1:2018 kilichotolewa na Shirika la Viwango la Uingereza (BSI) kwa Benki ya CRDBBenki ya CRDB. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA Benki ya CRDB, Mwanaisha Kejo.






Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA