Dar es Salaam. Tarehe 16 Januari 2024: Katika kuimarisha uwezo wake na ushirikishaji wa wadau, Taasisi ya CRDB Bank Foundation imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Mkataba huo wa miaka mitano unakusudia kufanikisha uwezeshaji wananchi hasa wajasiriamali vijana na wanawake, upatikanaji rahisi wa mtaji wa kukuza na kuendeleza biashara, ukuzaji wa biashara changa za kibunifu pamoja na kubadilishana uzoefu.
Ushirikiano huu wa kimkakati kati ya Taasisi ya CRDB Bank Foundation na UNDP unadhihirisha juhudi za pamoja zinazolenga kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuwezesha ukuaji jumuishi wa uchumi na utekelezaji wa Malengo Endelevu nchini.
Makubalino haya yanafungua milango ya utekelezaji wa miradi ya kuwezesha usawa wa kijinsia katika fursa za uchumi na biashara, kuwajengea vijana uwezo, ujumuishaji wananchi katika huduma za fedha, na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ikiwa na zaidi ya biashara changa, ndogo na za kati milioni 3 zinazochangia asilimia 27 kwenye pato la taifa (GDP) huku nyingi zikimilikiwa na wanawake, Tanzania ina nafasi nzuri ya kunufaika zaidi na ushirikiano wa kimkakati kama huu ulioingiwa kati ya Taasisi ya CRDB Bank Foundation na UNDP kwa kuwawezesha wananchi hasa vijana na wanawake wajasiriamali kunufaika na fursa zilizopo katika Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Akizungumza katika hafla ya kutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Ether Mwambapa amesema biashara changa, ndogo na za kati zina mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa na kipato cha mwananchi mmojammoja hivyo kuhitaji mkakati makini wa kuzilea na kuzikuza.
“Uchumi wa taifa letu unazitegemea biashara changa, ndogo na za kati kwa kiasi kikubwa. Sekta hii inaajiri zaidi ya watu milioni 5 hawa vijana na wanawake ambao hawawezi kuzifikia fursa za kiuchumi zilizopo sokoni.
Kwa kulitambua hili, Taasisi ya CRDB Bank Foundation ilibuni na kuitambulisha Programu ya Imbeju inayowaelimisha vijana na wanawake namna ya kuendesha biashara kisasa na kutoa mtaji wezeshi.
Kushirikiana na UNDP kunadhihirisha utayari wetu wa kuyabadili na kuyaboresha maisha ya mjasiriamali wa Tanzania tukiuanza mwaka mpya, 2024,” amesema Tully.
Mkurugenzi huyo amesema tangu Programu ya Imbeju ilipozinduliwa mapema mwaka jana, tayari mafunzo yaliyotolewa yamewanufaisha zaidi ya wanawake 100,000 huku mtaji wezeshi wa zaidi ya shilingi bilioni 5 ukiwa umetolewa kwa wajasiriamali waliokidhi vigezo.
Mkataba huu wa makubaliano pia unaendana na malengo ya Taasisi ya CRDB Bank Foundation katika kutekeleza Malengo Endelevu ya Dunia (SDG) hasa lengo namba 1 linalolenga kuondoa umasikini, lengo namba 5 linalohamasisha usawa wa kijinsia pamoja na ajira kwa wote kama ilivyoainishwa kwenye lengo namba 8.
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Shigeki Komatsubara amesema wakati wote, shirika hilo linajielekeza kufanikisha utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia. “UNDP inafanya kila iwezalo kuwezesha utekelezaji wa malengo endelevu kwa kuweka mazingira rafiki ya kuimarisha kipato, kuwa na jamii inayojitegemea na kuhamasisha utawala bora.
Mambo haya ndio yanayojenga msingi wa matendo yetu hivyo ushirikiano huu tunaousaini leo unaonyesha utayari wetu wa kufungua fursa kwa wananchi,” amesema Komatsubara. Katika kuyafikia malengo, Komatsubara amesema ni muhimu kuwa na ushirikiano wa wadau wenye maono sawa.
“Tukiianza safari hii ya ushirikiano, ni furaha kuona kuwa tunaelekea kwenye kutimiza ndoto ya kuacha alama kwa kuchangia mabadiliko chanya kwa jamii. Ushirikiano unaozihusisha taasisi kubwa ni muhimu ili kujenga misingi ya kesho iliyo sawa kwa wote, endelevu na yenye uchumi shirikishi,” amesema Komatsubara.
Ushirikiano wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation na UNDP ambazo zote zinazo programu zinazowalenga vijana na wanawake, unatarajiwa kufungua fursa nyingi zaidi kwa wajasiriamali wadogo wa Tanzania hasa vijana na wanawake kunufaika na soko pana lililopo ndani ya AfCFTA. Wakati Taasisiya CRDB Bank Foundation ikiwa na Imbeju, UNDP inao mradi wa Funguo unaowajengea uwezo vijana wabunifu.
Post a Comment