KAMATI YA BUNGE YAISHAURI TAMISEMI USIMAMIZI WA MIRADI YA ELIMU


Na. Asila Twaha, Morogoro


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) imeshauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI kusimamia miradi ya elimu kwa kushirikisha wataalamu wenye taaluma kulingana na mradi husika ili kuangalia ubora wa miradi  na ikamilike kwa wakati. 


Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Denis Londo ameyasema hayo  Februari 19, 2024  kwenye ziara ya kikazi  ya kukagua ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana iliyojengwa Mkoa wa Morogoro Halmashauri ya Wilaya Morogoro Kata ya Mvuha.


Mhe. Londo amemtaka Katibu Mkuu TAMISEMI kuipatia Kamati hiyo muhtasari wa vikao vilivyofanyika vya maamuzi ya kujenga shule hiyo katika eneo hilo, kuangalia tena ubora na utekelezaji wa ujenzi na pia kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kushirikiana na wataalamu wake kuonesha tofauti ya maendeleo ya ujenzi huo.


Naye, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI,  Sospeter Mtwale ameiahidi Kamati hiyo kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri walioutoa kwa manufaa ya wananchi.


Awali, akisoma taarifa ya ujenzi  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro,  Joanfaith Kataraia  amesema sh.Bilioni 3 zilipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa sekondari ya wasichana na utekelezaji umefanyika kwa kutumia force account ambapo vifaa vya ujenzi hununuliwa na Halmashauri kupitia kamati zilizoundwa na ujenzi hufanywa na mafundi walioajiriwa katika majengo mbalimbali kulingana na mikataba yao.


Hata hivyo, ameeleza  changamoto mbalimbali  katika ujenzi wa shule ikiwemo ya ukosefu wa maji ya kutosha katika eneo la ujenzi huku akieleza hatua zilizochukuliwa za uchimbaji wa kisima kirefu ili kuweza kukidhi mahitaji ya maji katika eneo la ujenzi na kuendelea na kazi na kwamba mradi huo ukikamilika utaweza kupanua wigo wa fursa ya wanafunzi kupata elimu.







 

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA