MAFUNZO YA TGNP YAWEZESHA WANAWAKE KILOLELI KUINUKA KIUCHUMI..WAANZISHA KIWANDA CHA BIDHAA ZA NGOZI


Na Mapuli Misalaba - Kishapu

Kikundi cha Kalangale kilichopo kata ya Kiloleli Halmashauri ya Kishapu kinachotekeleza mradi wa kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa za ngozi kimeishukuru Serikali pamoja na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa mchango wao katika kufanikisha mradi huo

Kikundi ambacho kina wanachama 17 ambao ni wanawake na  
wanaume kimetoa pongezi hizo leo wakati kikionesha bidhaa wanazotengeneza baada ya kujengewa uwezo na TGNP ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.

Makamu Mwenyekiti wa kikundi hicho Bi. Regina Emmanuel Nyahigi amesema mradi huo wa kutengeneza bidhaa za ngozi ikiwemo viatu na mikoba umewasaidia kuinuka kiuchumi na kuondokana na hali utegemezi katika familia zao.

“Zamani kwenye familia zetu tulikuwa tunamtegemea tu mwanaume hata sisi Wanawake tulikuwa tunakata mkaa ili tupate chochote kuendesha familia ila sasa hivi tunajishughulisha hapa hatukati hata mkaa tunashukuru sana kwa mradi huu maana tunanufaika sana”,amesema

“Kwa sasa sisi wanawake tukiuza bidhaa zetu hela tunagawana, kwa hiyo nikipata gawio tayari hapo nimepata mahitaji ya kuweza kuendesha familia.  Tunawashukuru sana TGNP kwa sababu kabla ya mradi huu tulikuwa tukikopa kwa mtu kuirudisha hiyo hela mpaka tukakate miti tuchome mkaa, sasa hivi hatuna hofu tunafanya biashara yetu kwa kujiamini”,amesema Regina

Baadhi ya wajumbe wa kikundi hicho cha kutengeneza bidhaa za Ngozi wameushukuru mtandao wa Jinsia TGNP kwa kuendelea kuwawezesha katika nyanja mbalimbali ikiwemo ubunifu pamoja na uibuaji wa miradi.

Wameeleza kuwa, kikundi cha Kalangale kimeanzisha mradi wa kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa za Ngozi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga baada ya kupata mafunzo maalum kutoka Mtandao wa Jinsia TGNP.

Pamoja na mambo mengine wamesema mradi huo umekuwa chachu pia kwao katika nafasi ya uongozi kwa wanawake ambapo wamekuwa na ujasiri kutoka na elimu mbalimbali wanazozipata.

Mmoja wa wajumbe wa kikundi hicho ambaye ni mnufaika kutoka kituo cha taarifa na maarifa Kiloleli Joseph Soleya amesema mradi wa kutengeneza bidhaa za ngozi umekuwa sehemu ya ajira hasa kwa vijana ambapo wanasambaza bidhaa hizo kwenda kuuza sehemu mbalimbali ili kujipatia kipato.

Kwa upande wake Katibu msaidizi wa kituo cha taarifa na maarifa Kiloleli ambaye pia ni mjumbe wa kikundi hicho cha kuchakata Ngozi,  Zakaria Pimbi amesema mradi huo umeanza rasmi mwaka 2021 ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia nchi Vijijini (EBBAR) walikiwezesha kikundi hicho kiasi cha fedha Sh. milioni 95.6 na kuanzisha Kiwanda hicho cha kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi.

Mradi huo upo katika kijiji na kata ya Kiloleli na kwamba umelenga kuinua uchumi wa wananchi kwa kuhakikisha wanapata kipato mbadala badala ya kutegemea kipato kutokana na rasilimali za misitu kama kuchoma mkaa na kuuza kuni kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia Nchi.
Katibu msaidizi kutoka kituo cha taarifa na maarifa  Kiloleli Kishapu ambaye pia ni mjumbe wa kikundi hicho cha kuchakata ngozi Bwana Zakaria Pimbi akielezea manufaa ya mradi huo.
Mmoja wa wajumbe wa kikundi hicho ambaye ni mnufaika kutoka kituo cha taarifa na maarifa , Joseph Soleya akiishukuru TGNP.
Mjumbe wa kikundi hicho Martha Ngwelu akielezea fursa zilizopatikana kutoka na mafunzo ya uongozi kwa wanawake huku akishukuru kwa mafunzo ya TGNP.
Wana kikundi cha Kalangale kinachotekeleza mradi wa kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa za Ngozi kijiji cha Kiloleli Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wakionesha bidhaa wanazotengeneza.
Wana kikundi cha Kalangale kinachotekeleza mradi wa kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa za Ngozi kijiji cha Kiloleli Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wakionesha bidhaa wanazotengeneza.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo akiendelea na shughuli ya utengenezaji bidhaa zitokanazo na ngozi.
Bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa katika kiwanda hicho kidogo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa katika kiwanga hicho kidogo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA