SERIKALI YAJA NA MWAROBAINI MGOGORO WA ARDHI RUSUMO ULIODUMU KWA MUDA MREFU NGARA MKOANI KAGERA


Na, Mwandishi Wetu - Dodoma.

Serikali kupitia Jeshi la Magereza imeendelea kuchukua hatua mbalimbali vikiwemo vikao vya ujirani mwema, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kwa ajili ya kushughulikia mgogoro wa Ardhi kati ya Gereza la Rusumo na Wananchi wa Kijiji cha Rusumo Mkoani Kagera.


Majibu hayo ya serikali yametolewa na Naibu waziri waa mambo ya ndani ya nchi Mhe. Daniel Sillo kufuatia swali la Mbunge wa Jimbo la Ngara Mhe. Ndaisaba Ruhoro leo Juni 26, 2024 bungeni jijini Dodoma alilouliza kuwa "Je, lini Serikali itatatua mgogoro wa Ardhi kati ya Gereza la Rusumo na Wananchi wa Kijiji cha Rusumo.?' 


Mhe. Sillo amebainisha kuwa Gereza kilimo Rusumo hilo lenye ukubwa wa ekari 9,442.9 (Hekta 3821.411) limepimwa na kupata hati Na.5548 katika mwaka 2023 hivyo serikali inatambua changamoto ya uhitaji wa ardhi kwa wananchi wa kijiji cha Rusumo.


"Serikali kupitia Jeshi la Magereza inatambua changamoto ya uhitaji wa ardhi kwa wananchi wa kijiji cha Rusumo na kilichopo ni wananchi kudai majira ya nukta za upimaji (Coordinates) ya Gereza Rusumo uliofanywa na Halmashauri ya Wilaya Ngara uliopitiliza hadi kwenye barabara na maeneo ya hifadhi ya mto Kagera." Amesema Naibu Waziri huyo


Kufuatia majibu hayo ya Serikali yakamuibua Mbunge huyo kuuliza swali la nyongeza la kutaka kujua ni lini serikali itafika eneo la tukio imalize mgogoro huo ambapo kwa mujibu wa Serikali matatizo ya nukta yalitokana na magereza kufanya upimaji bila kuhusisha kijiji na wananchi wanaoishi maeneo hayo.


Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa Jeshi la Magereza wataalamu watangulie kupima ili wakifika waweze kupata mwarobaini wa mgogoro huo wa muda mrefu.


"Niko tayari kuambatana na Mbunge baada ya Bunge la Bajeti tutapanga utaratibu mzuri ili tuende tukasikilize changamoto hii lakini pia nitoe Wito kwa Jeshi la Magereza kuwa wataalamu wetu watangulie waanze kupima ili tukifika tuweze kumaliza changamoto hii ya muda mrefu" Amesema Mheshimiwa Sillo.









Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA