TUONE UMUHIMU WA KUCHANGIA DAMU HAKUNA MBADALA WAKE

 

John Francis Haule

Kila ifikapo Juni 14 dunia huadhimisha siku ya mchangia damu. Katika siku hii hamasa huwa kubwa zaidi lakini ukweli ni kwamba suala la uchangiaji wa damu halina siku maalumu kutokana na umuhimu wake.

Nasema hivi kwa sababu hakuna mbadala wa damu inahitajika kila siku. Damu ni tiba muhimu kwa afya ya mwanadamu na ni damu ya binadamu pekee ndio inayotumika.

Kutokana na umuhimu huo, tuna kila sababu kuhakikisha wakati wote inapatikana na upatikanaji wake ni lazima tujitoe kwa kuwa damu hainunuliwi wala haitengenezwi maabara kama ilivyo dawa nyingine.

Damu mahitaji yake ni makubwa sana na upatikanaji wake ni waasili maana kwamba hakuna kiwanda kinacho chakata damu, ni sisi binadamu tunapaswa kushiriki tendo hili la huruma la kuchangia damu kwa hiari.

Matumizi ya damu nchini ni makubwa kwa akina mama wajawazito wanaopoteza damu wakati wa kujifungua, watoto wenye umri chini ya miaka 5, wahanga wa ajali za barabarani na wagonjwa wa saratani. 

Tunafahamu kila uchao zinatokea ajali za barabarani ambazo zinaacha majeruhi wanaohitaji damu, ili kuokoa maisha yao ni lazima tuwe na akiba ya kutosha kwenye benki za damu katika hospitali zetu.

Tunaambiwa kuwa upungufu wa damu unaweza pia kugharimu maisha ya mjamzito na kiumbe kilichopo tumboni mwake. Hii ina maana kuwa mchakato wa kuleta uhai wa mtu mwingine damu ina umuhimu mkubwa.

Takwimu zinaonesha takribani  asilimia 19 ya wanawake wajawazito wanapoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na kuvuja damu nyingi.

Hivyo kila mwananchi mwenye afya njema ni muhimu akajitolea  kuchangia damu ili kuhakikisha akiba  ya damu inadumishwa ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji hasa katika kuunga mkono ajenda ya kupunguza vifo vya wajawazito nchini Tanzania.
Kutokana  na changamoto hiyo ni muhimu benki za damu katika hospitali zote nchini kuwa na damu ya kutosha ili kukabiliana na dharura za aina hiyo zinapojitokeza.

Swali linakuja benki za damu zinatoa wapi ilhali tumekubaliana kuwa hakuna kiwanda wala mtambo wa kuzalisha damu, jibu ni kwamba ni lazima tuwe na utaratibu wa kudumu wa kujitolea damu.

Usilazimike kuchangia damu kwa sababu kuna ndugu yako au mtu wako wa karibu amelazwa hospitali, jenga utamaduni huu kwa kuwa damu yako inaweza kuokoa maisha ya mtu mwingine kabisa.

Kwa umuhimu huo nimeona kuna haja ya kutumia ushawishi wangu na watu wanaonizunguka katika mazingira yangu ya kazi kuhamasisha uchangiaji damu wa hiari na kuwajengea Watanzania desturi hii ambayo ina maana kubwa kwa Mungu.

Pia nishauri wale tuliopewa dhamana ya kuongoza ama kusimamia maeneo yenye  mkusanyiko wa watu wengi  tutumie hio fursa kuhamasisha jamii kuwa na desturi  ya kuchangia damu, mfano vyuoni,kwenye makongamano ya dini.

Kila mchango wa damu  ni zawadi ya thamani inayookoa uhai na uchangiaji wa kurudia ndio ufunguo wa kujenga usambazaji wa damu salama na endelevu.

Mwandishi wa Makala hii John Francis Haule (Mkuu wa soko kuu la Arusha anapatikana kwa simu namba  0711 993 907 au 0756717987


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA