Na Mwandishi wetu
MGOMBEA wa urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), Sweetbert Nkuba amesema hakubaliani na matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Kamati ya uchaguzi ya chama hicho hapo jana na amejipanga kupeleka pingamizi mahakamani.
Amesema tayari amewaagiza wanasheria wake kwenda mahakamani kupinga uchaguzi huo.
Amesema anaamini kwamba uchaguzi huo 'umechakachuliwa' kwa sababu pamoja na kamati ya uchaguzi kufahamu idadi ya wapigakura lakini haikupeleka karatasi za kutosha za kupigia kura na hivyo kulazimika kwenda kuchapisha nyingine wakati uchaguzi ukiendelea.
Sababu ya pili anasema katika makubalianao yao, ilikuwa ni kwamba mawakala wasiingie na vifaa vya mawasiliano kwenye chumba cha kuhesabia kura, lakini katika hali ya kushangaza matokeo yasiyo rasmi yalianza kuvuja kabla ya kutangazwa kwa matokeo rasmi.
"Kwa hiyo tunaamini kwamba hizi ni hujuma za kamati ya uchaguzi ama kamati imeshirikiana na watu kuwapenyezea matokeo yasiyo rasmi na kuyatangaza nje na baadae watu hawa wamefanya vurugu za kwenda kushinikiza kamati kutangaza matokeo wanayoyataka wao,"anasema Nkuba.
"Kwa hiyo mimi naamini kamati imekosa weledi, msimamo na imehusika katika kuhujumu au kunajisi mchakato mzima wa uchaguzi kwa kutangaza matokeo ambayo hayaakisi uhalisia wa wapigakura na ubora wa kampeni na ubora wa zoezi lilivyokwenda."
"Kwa taarifa hii, naomba kuujulisha umma kwamba njnakwenda mahakamani kupinga mchakato huu wa uchaguzi na kupinga matokeo na kubatilisha ushindi uliotangazwa na kamati ya uchaguzi, naamini mahakama itasimamia haki na kuufuta uchaguzi huu ili kuitisha uchaguzi mpya kwa ajili ya kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanyika kwa viwango na kwa kuzingatia weledi na usawa wa pande zote."
Katika uchaguzi huo uliofanyika jana, Kamati ya uchaguzi iliyosimamia uchaguzi huo wa TLS ilimtangaza Boniface Mwabukusi kuwa ndiye mshindi kati ya wenzake watano waliokuwa wakiwania kinyang'anyiro hicho.
Wagombea wengine walioshindana katika nafasi hiyo ya urais ni Emmanuel Muga, Paul Kaunda, Revocatus Kuuli na Kapteni Ibrahim Bendera
Post a Comment