Na, Dotto Kwilasa - Dodoma.
Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linamshikilia Raphael Keneth Ndamahnuwa mwenye umri wa miaka 26,Mlinzi Mkazi wa Nzuguni B kwa mahojiano kuhusiana na tukio la kifo cha mwanamziki Joseph Francis Michael maarufu kama Man'dojo (46).
Hatua hii imekuja kufuatia Mwanamziki aliyewahi kutamba na kibao cha Wanokunoku kwa kushirikiana na Lady Jay Dee,Mandojo kufariki dunia kwa kupigwa na mtu anayedhaniwa kuwa mlinzi wa kanisa Katoliki na kupelekea kifo chake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 13,2024 Jijini Dodoma Kaimu Kamanda wa Polisi,Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi,Anania Amo ameeleza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na daktari ili kubaini chanzo cha kifo chake.
Amefafanua kuwa Mandojo alifariki akiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kutokana na kipigo alichokipata baada ya kutuhumiwa kuwa ni mwizi akiwa eneo la Nzuguni B
"Mnamo Agosti 11,majira ya saa 12:00 mchana huko katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Joseph Francis Michael maarufu kama Man'dojo miaka 46 Mkulya mwanamziki Mkazi wa Nzuguni B alifariki,akiwa anaendelea na matibabu"amesema
Kaimu Kamanda huyo amesema kifo cha Mwanamziki huyo kimesababishwa na kushukiwa kuwa ni mwizi baada ya kukutwa ndani ya uzio wa Kanisa Katoliki Parokia ya Watakatifu wote lililopo Nzuguni B ambapo alikutwa akiwa amejificha katika banda la mbwa.
"Marehemu akiwa kwenye banda hilo mlinzi wa eneo hilo alisikia mbwa wanabweka kwa nje ya kibanda chao na alipofika eneo hilo aligundua kuna mtu amejifungia ndani ya chumba kimojawapo cha banda hilo," amefafanua.
Mbali na tukio hilo Kaimu Kamanda wa Polisi Anania Amo ametoa wito kwa wananchi Mkoa wa Dodoma kuacha kujichukulia Sheria mkononi kwani kufanya hivyo ni kinyume na Sheria za nchi.
"Niwasihi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye vyombo husika ili wachukuliwe hatua stahiki, kinachotakiwa ni kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, " amesisitiza
Wakati huu huo amesema,Jeshi hilo linaendelea na msako wa wahalifu kila Kona na kwamba atakaebainika anafanya uhalifi atachukuliwa hatua kali za kisheria huku akisisitiza kuwa Jeshi hilo limekuwa likifanya msako wa kutafuta wahalifu na kuwachukulia hatua za kisheria pale wanapofanya makosa mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo imefanya mahojiano na baadhi ya mashabiki wa Mandojo ambapo wameeleza masikitiko yao kuhusu kifo chake kwa namna ya kipekee, wakisema kuwa kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya muziki.
Ali Kimasi amesema kuwa Mandojo alikuwa na kipaji cha pekee na mchango wake katika muziki utaendelea kuishi kwa muda mrefu na kupongeza mchango wake kwa jamii na kutoa pole kwa familia yake na wapenzi wake wote.
Post a Comment