RAIS SAMIA AMEIBEBA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KIMATAIFA - DKT. BITEKO

 


Imeelezwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia nchini na Afrika bado anaendelea kuipeleka ajenda hiyo Kimataifa ili kuhakikisha watu wanapika katika mazingira salama kiafya na kimazingira.

 

Hayo yamebainishwa leo Agosti 23, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko katika Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia ambalo limeandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) na Benki ya Uwekezaji ya Tanzania (TIB) kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi zote za Serikali lililofanyika katika Hoteli ya Kwanza, Kizimkazi Zanzibar.


Amesema kuwa, suala la nishati safi ya kupikia imekuwa ni ajenda muhimu nchini na duniani kote na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa ajenda hiyo Afrika kwa kuibeba kuanzia mwezi Novemba 2022.


Dkt. Biteko amesema lengo  la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapika katika mazingira salama na kwamba  hatua hii itawezekana kwa kupatikana kwa nishati safi ya kupikia  iliyo nafuu, inayopatikana na kutumika kwa urahisi.


"Matarajio yetu ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia. Nimefarijika sana kuona utekelezaji wa lengo hili kwa vitendo, nimeona teknolojia mbalimbali katika mabanda ya maonesho hapo nje na niendelee kuhamasisha ubunifu wa teknolojia zinazowezesha wananchi kupata nishati safi kwa gharama nafuu." Amesema Dkt. Biteko


Amesema Wizara ya Nishati itaendelea kutoa kipaumbele ajenda hiyo kwa namna mbalimbali ikiwemo kuanzisha Kitengo maalum cha usimamizi wa nishati hiyo.


Vile vile,  Dkt. Biteko amewapongeza wabunifu kutoka banda la ORXY ambao wamekuja na ubunifu kwenye mitungi ya gesi (LPG) kwa kuweka mita inayopima gesi ambayo inarahisisha gharama za kujaza gesi na kuwa nafuu zaidi.


Pia, ametoa wito kwa viongozi wote wa Serikali, Siasa, Dini na wa Jadi waliopo katika maeneo mbalimbali kuunga mkono ajenda hiyo yenye nia njema ya kumkomboa kila Mtanzania na kwamba kwenye majukwaa yao, wasiliache nyuma suala hilo. 


"Tuhakikishe watu tunaowaongoza wanaelewa vyema umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kwa kampuni zinazowajibika katika jamii zao kupitia Corporate Social Responsibilities (CSR) niwahimize kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mkakati kwa vitendo kwa kugawa vifaa vya nishati safi ya kupikia kwa wenye uhitaji. Naamini tukishirikiana wote kwa pamoja tutaweza." Amesema Dkt. Biteko. 


Halikadhalika amesema, takriban watu bilioni 2.4 hawatumii nishati safi duniani, kati ya hao milioni 933 wanatoka Afrika na kwa mwaka duniani watu milioni 3.7 wanakufa na vifo ni asilimia 60 wakiwemo wanawake na watoto. 


Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Mhe. Ayoub Mohammed Mahamoud, amesema suala la Nishati Safi ya Kupikia sasa ni ajenda ya Kimataifa na wataibeba katika kutoa elimu na kuelimisha umma kususu matumizi salama ya nishati hiyo kwa upana


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), Wanu Hafidh Ameir amesema Nishati safi ya Kupikia imekuwa ni mkombozi kwa wanawake na kulinda Afya zao.


 Amewataka watanzania kutumia nishati hiyo ambayo ni mkombozi wa utunzaji wa mazingira na kiuchumi nchini. 


Tamasha la Kizimkazi mwaka 2024, limesheheni vitu vingi ikiwemo ufunguzi wa miradi mbalimbali ikiwemo kiwanja cha Suluhu Academy.

 






Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA