TALGWU WAISHUKURU SERIKALI KWA KUBORESHA KIKOKOTOO, WATOA WITO HUU KUELEKEA UCHAGUZI

 


Wafanyakazi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) waliopata fursa ya kushiriki zoezi la uboreshaji wa daftari la Wapiga kura kuelekea uchaguzi wametakiwa kufanya kazi yao kwa weledi na kutokutumika kisiasa.



Wito huo umetolewa leo Agosti 16, 2024 na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania  TALGWU Mkoa wa Dodoma Ndg. Audax Stephano Stanslaus katika kikao  kilichowakutanisha wanachama ambao pia ni Maafisa utumishi kutoka Maeneo Mbalimbali Mkoani Dodoma.


Katibu huyo amesisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia kanuni na miongozo kwa afya ya siasa Nchini ili kuendelea kudumisha amani iliyopo huku miongoni mwa adhabu anayoweza kukutana nayo mwanachama kwa utovu wa nidhamu ni pamoja na kufutwa uanachama.

"Nitoe rai kwa wafanyakazi wote wa Mkoa wa Dodoma ambao watahusika katika zoezi la kurekebisha daftari la kupiga kura na kusimamia uchaguzi wajitahidi kufanya kazi kwa weledi na umakini mkubwa pasi na kuingia kwenye miibuko ya kisiasa" Alisema Ndg. Audax Stanslaus

"Chama cha wafanyakazi (TALGWU) hakitetei maovu na siyo sehemu ya siasa na hakina Chama cha siasa hivyo wafanyakazi wake wajitahidi kuzingatia kanuni na weledi ili wabaki salama na Nchi hii inasifika kwa utawala bora" Alisema Katibu Ndg. Audax Stanslaus

Katika hatua nyingine ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha Chama hicho (Kikokotoo) kwa kuongeza mishahara ya wafanyakazi nchini kwani wanaimani kubwa na wanatamani maboresho yaendelee kufanyika kulingana na muda unavyozidi kwenda.


Aidha wamewasilisha ombi kwa serikali kuangalia kwa jicho la tatu wafanyakazi wanaoenda masomoni na baada ya kurejea makazini kukumbana na changamoto ya kushushiwa mishahara yao.

"Tunaomba huu Mfumo uangaliwe upya kuna wafanyakazi wameenda masomoni kwaajili ya kuboresha ujira wao lakini wanapotoka masomoni mishahara yao inashuka, Si dhambi kama mtu amejiendeleza ndani ya kada yake na kazi ni zilezile katika kituo hakuna sababu ya kumshusha mshahara kwa kigezo cha kusoma" Alisema Ndg. Audax Stanslaus

"Inaumiza sana ninayo mifano katika Mkoa wangu, huu mfumo uangaliwe upya wa mfanyakazi aliyetoka kujiendeleza kama inawezekana baada ya kurejea waendelezwe katika mishahara yao na vyeo walivyonavyo" Alisema Katibu huyo

Subira Abdallah Said akizungumza kwa niaba ya Wanachama walioshiriki amewataka watumishi wote nchini kujiunga na Chama hicho kwani pindi wakutanapo na changamoto za kazi inakuwa rahisi kutatuliwa yeye akiwa ni shuhuda kwani ni miongoni mwa wanufaika na anaamini kero aliyoiwasilisha katika Kikao hicho cha leo itatatuliwa kwa wakati.

 


 


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA