VYUO VIKUU VYA TANZANIA VYAAHIDI KUENDELEZA UWEZESHAJI WA WANAWAKE KIUCHUMI


Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa, Mhe. Anjellah Kairuki akizungumza kwenye mkutano huo

Makamu wakuu wa vyuo vikuu nchini Tanzania wameahidi kuuunga mkono juhudi za kitaifa za kuharakisha utekelezaji wa ahadi za kujenga kizazi chenye usawa. 

Katika kongamano la ngazi ya juu lililoandaliwa tarehe 8 Oktoba 2024 jijini Dar es Salaam, Makamu Wakuu wa Vyuo na wawakilishi wa Vyuo Vikuu vya Tanzania wamejadiliana na Wizara ya Elimu na Jukwaa la Kitaifa la Ujenzi wa Kizazi Chenye Usawa wa Kizazi (GEF) na kuona namna ambavyo Vyuo Vikuu vinavyoweza kuoanisha mipango na kazi kukuza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. 

Mkutano huo ni mfululizo wa matukio mikutano ya wadau yenye lengo la kujenga uelewa  na kupanga utekelezaji wa ahadi za kimataifa za Tanzania zilizotolewa mwaka 2021. Mikutano ilishirikisha mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya kiraia, sekta ya kibinafsi na mtandao wa kitaifa wa vituo vya wavumbuzi.

Akizungumza kwenye mkutano huo wenye  lengo la kuangazia "Kuimarisha Wajibu wa Wasomi katika Kuharakisha na  Kukuza kuiwezesha jamii kuzifahamu na kuzitekeleza ahadi za Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa (GEF)", Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa, Mhe. Anjellah Jasmin Kairuki amesema Vyuo vikuu vina jukumu muhimu katika kukuza usawa wa kijinsia kwa kutumia utafiti kushawishi sera na kukuza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ili kuleta matokeo chanya sawa.
"Taasisi za kitaaluma zinaweza kuziba mapengo katika sera, programu na takwimu za jinsia kupitia utafiti wa kina, tafiti za uchambuzi na kuongeza uwezo wa utafiti," amesema Mwenyekiti wa GEF Tanzania, Mheshimiwa Angellah Kairuki.

Ameongeza kuwa Kituo cha Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi cha Chuo Kikuu cha Kenya kimefaulu kutoa ushahidi na kuongoza juhudi za utetezi ambazo zilileta maendeleo makubwa katika uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

"Tunaamini kwamba vyuo vikuu vyetu nchini Tanzania vinaweza kujifunza na kuweka mipango yao madhubuti ya uwezeshaji inayozingatia muktadha wa  nchi yetu. Jumuiya ya wasomi ina jukumu muhimu katika kuunda mawazo ya viongozi wa baadaye, kufanya tafiti muhimu, na kuunda majukwaa ya uvumbuzi. Nguvu ya kielimu  inapotumika katika uhalisia wa jamii yetu, huleta matokeo chanya",amesema .

Jukwaa la Usawa wa Kizazi (GEF) lililoundwa mwaka 2021 baada ya miaka ishirini na mitano ya Jukwaa la Beijing, linahakikisha utekelezaji kamili wa malengo usawa wa jinsia na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyokubaliwa na serikali ya Tanzania, pamoja na mashirika mengine na dunia kwa ujumla.

Tanzania imepunguza kwa kiasi kikubwa pengo la kijinsia katika uandikishaji wa wavulana na wasichana katika elimu ya msingi na sekondari na, imeongeza uandikishaji wa wanawake katika vyuo vikuu vya elimu ya juu. Hata hivyo, ushiriki wa wanawake katika uongozi wa utafiti na sayansi na teknolojia bado uko chini.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum,bi Felister Mdemu amesema Programu ya Kizazi Chenye Usawa ni muendelezo wa utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing la Mwaka 1995 ambapo inalenga katika kuongeza chachu miongoni mwa jamii ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na Azimio hilo sambamba na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Sustainable Development Goals 2030).

Amesema Taasisi za Vyuo Vikuu zina mchango mkubwa na ni ndio kitovu cha tafiti mbalimbali ambazo ni muhimu katika kupanga mipango na kuandaa sera ambazo ni jumuishi. 

“Naamini kwa ushirikiano wa pamoja tutaweza kutekeleza Ahadi za nchi kwenye Jukwaa hilo sambamba na kumuwezesha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni kinara wa Jukwaa hilo kuendelea kung’ara”,ameongeza .

Wawakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta na Chuo Kikuu cha Nairobi wamewasilisha mafanikio yao kwenye kongamano hilo la Makamu wa Vyuo Vikuu Tanzania. 

Maeneo ambayo vyuo vikuu vinaweza kuwekeza katika uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni pamoja na kubuni mafunzo yanayozingatia jinsia katika mitaala, kuandaa programu za msaada wa kitaaluma kwa wanafunzi wa kike ili kuwatayarisha kwa ajili ya majukumu ya uongozi na kuingia katika tasnia mbalimbali.

Maeneo mengine ni kuanzisha ufadhili wa masomo na programu za mafunzo kwa wanawake katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati, na kusaidia ushiriki wao katika miradi ya utafiti na uvumbuzi.
Msukumo wa usawa wa kijinsia katika taasisi za elimu ya juu unajenga kwenye mafanikio yaliyopo, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa pengo la kijinsia katika uandikishaji. Kadhalika, miradi ya utafiti inayoongozwa na wanawake imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka 12.6% kati ya 2011 na 2015 hadi 50% mwaka 2021 hadi 2024, kulingana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania.

Kwa kuzingatia mafanikio haya, vyuo vikuu vinatarajiwa kuunganisha malengo ya GEF katika shughuli za kitaaluma na utafiti za chuo kikuu, kuendeleza mpango wa utekelezaji wa ushirikiano wa kutekeleza vituo vya uvumbuzi unaozingatia jinsia katika vyuo vikuu na kuimarisha uhusiano kati ya vyuo vikuu na wadau wanaofanya kazi kukuza usawa wa kijinsia.

Desemba 2021, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ili kutoa mwongozo wa utekelezaji wa ahadi za Usawa wa Kizazi cha Tanzania, inayowashirikisha viongozi 25 mashuhuri (wengi wao wakiwa wanawake) kutoka sekta mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar, inasukuma mbele ahadi zetu za Usawa wa Kizazi. Rais Samia Suluhu Hassan ameunda Kamati hii ili kusimamia na kuongoza utekelezaji wa malengo yetu kabambe ya haki na haki za wanawake kiuchumi.

Ifikapo mwaka 2026, Tanzania inalenga kuongeza uwekezaji katika huduma zinazozingatia jinsia, kuunda mifumo ya kisheria na sera inayounga mkono, kuimarisha upatikanaji wa rasilimali kwa wanawake, na kubuni sera za kiuchumi ili kupunguza umaskini miongoni mwa wanawake na wasichana. Mtazamo huu wa jumla unaahidi maendeleo ya mabadiliko kwa usawa wa kijinsia!



Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA