WAZIRI MKUU MAJALIWA AZITAKA WIZARA, TAASISI KUUPA UMUHIMU MKUTANO WA WADAU WA LISHE MAPAMBANO DHIDI YA UTAPIAMLO


Katika kuhakikisha Serikali, wadau wa afua za lishe na sekta binafasi wanaunganisha nguvu na kupata njia bora za kukabiliana na tatizo la utapiamlo na udumavu nchini, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka mawaziri wa kisekta, wakuu wa mikoa, wilaya, halmashauri na taasisi mbalimbali kuupa kipaumbele na kushiriki kwenye mkutano mkuu wa wadau wa lishe nchini ili kupata ushauri, maoni na mapendezo ya namna bora ya kukabiliana na tatizo hilo.

Majaliwa ametoa wito huo leo jijini Mwanza wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 10 wa Wadau wa Lishe nchini uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Oktoba 2-3, mwaka huu katika hoteli ya Malaika jijini Mwanza ukiwa na kaulimbiu ya ‘Kuchagiza mchango wa wadau wa kisekta ili kudumisha matokeo bora ya hali ya lishe nchini Tanzania’, huku akiwahakikishia wadau hao kuwa maoni, mapendekezo na ushauri uliotolewa kwenye mkutano huo yatafanyiwa kazi na Serikali.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda uliafikiana maazimio matano ambayo ni masuala ya huduma za lishe yajumuishwe katika dira ya taifa 2050 na kuimarisha huduma za lishe kwenye ngazi ya jamii ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hii, kuimarisha uratibu na utekelezaji wa vipaumbele vya Mpango wa Pili Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (Nutrition Multisecterial National Action Plan II - NMNAP II) kwa kuhakikisha kila Wizara za kisekta na wadau wa maendeleo wanawajibika kutekeleza afua za lishe kulingana na Mpango, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza afua za lishe, na kuimarisha upatikanaji na matumizi ya taarifa za lishe katika ngazi zote.

“Idadi ya wadau na wizara za kisekta zinatakiwa ziongezeke zihudhurie mkutano huu. Tamisemi, kilimo, afya, maendeleo ya jamii, mifugo na uvuvi zilete mawaziri waudhurie mkutano huu wapate maoni ya wadau na kufanya tathmini kuhusu utekelezaji wa afua za lishe, lazima wawepo kila mmoja apate jukumu lake, pia maafisa maendeleo wa halmashauri na maafisa lishe ili kushirikiana na wakuu wa wilaya na mikoa kutekeleza afua za lishe na mipango ya Serikali,” amesema Majaliwa.


Mkutano huo uliokuwa na kaulimbiu ya ‘Kuchagiza mchango zaidi wa wadau wa kisekta ili kudumisha matokeo bora ya hali ya lishe nchini Tanzania’ ulilenga la kudumisha dhamira ya pamoja ya Serikali na wadau katika kuongeza msukumo na uwekezaji katika kutekeleza Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe ili kukabiliana na changamoto za utapiamlo zinazoendelea katika jamii, na kupokea tathmini ya utekelezaji wa masuala ya lishe nchini kwa mwaka uliopita.

Majaliwa amesema takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa mwaka 2022 zinaonyesha theluthi moja ya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 wamedumaa, huku akiwataka wadau hao kutumia fursa ya mkutano huo kubadilishana uzoefu na mbinu zinazotumika katika utekelezaji wa programu za lishe nchini, ikiwa ni pamoja na ubunifu katika kukabiliana na changamoto za lishe.

“Ni dhahiri kuwa kila mmoja wetu anatambua kuwa lishe huathiriwa na mambo mbalimbali zaidi ya sekta ya afya. Hivyo, kwa kuhusisha wadau wa sekta kama vile kilimo, elimu, maji na usafi wa mazingira, na ulinzi wa kijamii, inawezesha kuweka mikakati endelevu ya kuboresha matokeo ya chanya ya lishe bora. Sababu kuu za kutilia mkazo ushiriki wa wadau wa kisekta wa lishe nchini Tanzania ni pamoja na kushughulikia sababu za msingi za utapiamlo kama vile umaskini, uhaba wa chakula, na mazoea duni ya utunzaji vyakula, pia kuboresha utumiaji wa rasilimali, kuunda ushirikiano na kujenga msingi madhubuti wa lishe,” amesema.

Naye, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda aliiomba Serikali kufikiria upya mpango wake wa kuipunguzia majukumu Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kwani imekuwa nguzo muhimu katika elimu na tafiti za lishe nchini, huku akishauri kushirikishwa kwa viongozi wa kimila na wa dini katika utoaji wa elimu ya lishe kwenye jamii kwani wana nguvu na ushawishi na itasaidia kuongeza uelewa na mapambano dhidi ya utapiamlo kufanikiwa.

“Nashukuru ninanapoona serikali inalivalia njuga suala hili kwa sababu wakati mwingine ni aibu na linatushushia hadhi kwa sababu ni jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu, naamini taratibu tutalichukulia kwa uzito mkubwa na kupunguza tatizo hili,” amesema Pinda.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema Serikali imeendelea kuhakikisha sekta zinazohusika na utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa masuala ya Lishe zinaingiza masuala hayo katika mipango na bajeti kila mwaka huku ofisi ya Waziri Mkuu ikiendelea kuratibu ufuatiliaji na tathmini pamoja na kuhakikisha wanawakutanisha mara kwa mara wadau kujadili utekelezaji wa afua za lishe nchini.

“Kwa takwimu tulizonazo sasa za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (2022) zinaonesha viwango vya udumavu na uzito mdogo (underweight) kwa watoto chini ya miaka mitano vimekuwa vikipungua. Katika kipindi cha mwaka 2018 na 2022 udumavu ulipungua kutoka asilimia 32 iliyokuwa mwaka 2018 hadi asilimia 30 kwa mwaka 2022, na uzito mdogo ulipungua kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 katika kipindi hicho. Jitihada za kukabiliana na changamoto hizi zimekuwa zikifanyika katika ngazi ya taifa na mkoa husika,” amesema Lukuvi


Meneja mradi wa kuhamasisha afua za Lishe kwa akina mama na watoto kwa kuangalia usawa wa kijinsia (Grow Enrich Project) kutoka World Vision Tanzania, Shukrani Dickson amesema ili kusaidia Serikali kukabiliana na changamoto hiyo, shirika hilo linafundisha akina mama ngazi ya jamii namna ya kuandaa mlo kamili kwa ajili ya watoto, kuhahakikisha kila mwaka watoto wanapata chanjo ya Vitamini A na kuwawezesha wahudumu wa afya kutembelea kaya kwa kaya ili kuwafundisha akina mama namna ya kuwatunza watoto na kuhudhuria kliniki na kupima watoto uzito.

“Tunao mpango mkubwa sana kama World Vision Tanzania kuhamasisha ulimaji wa viazi lishe, hivi viazi lishe na maharage lishe vinaongeza virutubisho vikubwa sana kwa watoto tunawahimiza wanajamii kulima viazi lishe kwa kuwapatia mbegu na utaalamu mbalimbali ili kuhakikisha kwamba watoto wanapata vyakula ambavyo vinaongeza virutubisho vinavyopatikana kwenye maeneo yao,” amesema Shukrani.


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Jesca Lebba amesema “Katika mkoa wetu wa Mwanza hali ya udumavu kwa sasa ni asilimia 28 Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 39 mwaka 2018. Kwenye uzito pungufu tuna asilimia 2.8 lengo la kitaifa ni asilimia tano lakini ukondefu ni asilimia 1.8 na lengo la kitaifa ni asilimia tatu nayo ukiangalia bado tunafanya vizuri,”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpa zawadi ya cheti na ngao Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka kwa kuwa kinara wa kupambana na utapiamlo, kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu William Lukuvi.

Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda akizungumza kwenye mkutano huo.
Wadau wa lishe wakifuatilia hotuba mbalimbali.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA