Taasisi ya Mwanyanya Green Society imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuboresha ubora wa elimu katika shule za msingi za Wilaya ya Kaskazini B, Zanzibar.
Mradi huu, unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Alwaleed Philanthropies, unalenga kuwajengea walimu uwezo kupitia mafunzo ya mbinu za kisasa za ufundishaji na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.
Shule zinazofaidika na mradi huu ni pamoja na Kiongwe, Pangatupu, Fujon, Mahonda, Mgambo, Kilombaro, Mgonjon, Hamid Ameir, na Mwanda. Mafunzo haya yanajumuisha walimu, wajumbe wa kamati za shule, na wazazi, yakilenga kuimarisha ushirikiano katika kukuza ubora wa elimu.
Uzinduzi rasmi wa mafunzo haya ulifanyika Novemba 23, 2024, katika Skuli ya Sekondari ya Mahonda, ambapo kituo cha ubunifu wa kisayansi, Mahonda HUB, kinatumika kama eneo la mafunzo. Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Mandalizi, Msingi na Kati, Bi. Fatma Ramadhan Mode, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Mafunzo hayo pia yamefanyika katika ukumbi wa walimu wa TC Mkwajuni, ambapo walimu wanajifunza mbinu za kisasa za ufundishaji pamoja na matumizi ya teknolojia ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Kupitia mradi huu, Mwanyanya Green Society inadhihirisha dhamira yake ya kuboresha sekta ya elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Mradi huu unatarajiwa kuleta athari kubwa kwa kuinua uwezo wa walimu na kuboresha kiwango cha elimu ya msingi katika Wilaya ya Kaskazini B, Zanzibar.
Post a Comment