Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) leo imepokea ziara ya Naibu Waziri Msaidizi ( Deputy Assistant Secretary, Bureau of International Narcotics And Law Enforcement) wa Shirika la Kimataifa la Dawa za Kulevya na Masuala ya Sheria (INL), Maggie Nardi, pamoja na ujumbe wake.
Ziara hiyo imelenga kuipongeza DCEA kwa mafanikio makubwa katika kudhibiti biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kuvunja mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kukamata kiasi kikubwa cha dawa hizo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Maggie Nardi alisifu juhudi za DCEA na serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Aliahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo ili kufanikisha vita dhidi ya janga hilo.
"Ninawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuvunja mitandao ya biashara ya dawa za kulevya na kukamata dawa nyingi. Ushirikiano wetu utaendelea kuimarika, na tunatoa pongezi kwa serikali ya Tanzania kwa jitihada zake madhubuti katika kukabiliana na changamoto hii," alisema Maggie Nardi.
Pamoja na pongezi hizo Maggie pia alifurahishwa na huduma za kupunguza uhitaji ya dawa za kulevya na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya.
"Sikufahamu kwamba DCEA pia inafanya kazi ya kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya pamoja na kupunguza madhara ya dawa hizo. Hii ni hatua nzuri ambayo inapaswa kuendelea," alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu tishio la dawa za kulevya, Nardi alielezea tishio linalotokana na dawa za kulevya za kisintetiki kama vile fentanyl, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na ushirikano wa habari ili kukabiliana na changamoto hii.
"Natumai fentanyl haijaingia kwa wingi hapa nchini, lakini lazima tuchukue tahadhari. Tunaendelea kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya biashara ya dawa za kulevya. Marekani ilijifunza kutokana na kile kilichotokea katika majimbo ya Kaskazini Mashariki, na hivyo walijitayarisha vyema wakati fentanyl ilipokuwa ikienea. Hii inadhihirisha umuhimu wa kushirikiana taarifa mapema." Alisisitiza Maggie.
Ziara hii ni ishara ya ushirikiano wa kimataifa unaozidi kuimarika katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, na DCEA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupambana na janga hili na kupunguza athari zake kwa jamii.
Post a Comment