WANANCHI KATA YA IHUMWA WAVUTIWA NA KASI YA UTENDAJI WA JESHI LA POLISI DODOMA

 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi akisikiliza kero za wananchi katika Kata ya Ihumwa -Dodoma

Na Mwandishi Maalum, DODOMA

Wananchi wa Kata ya Ihumwa Jijini Dodoma wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya watu wanaofanya uhalifu pamoja na vitendo vya ukatili kwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria hususani Mahakamani.

Hayo yameelezwa Disemba 11, 2024 katika Mkutano wa hadhara wa wananchi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi wakati akisikiliza Kero za wananchi hao juu masuala ya ulinzi na usalama katika kata ya Ihumwa ambapo aliambatana na watendaji wake.

Mbali na pongezi hizo kwa Jeshi la Polisi wananchi wa Kata hiyo wameomba hatua zinazochukuliwa ziwe endelevu ili iwe fundisho kwa wahalifu wengine kutokana na kudhibiti mtandao wa uhalifu ulikuwa ukijihusisha na vitendo vya ukatili vilivyokuwa vikileta taharuki katika eneo hilo.

Kamanda Katabazi amewataka wazazi na walezi kusimama imara katika malezi na kufuatilia mienendo ya watoto ili kuepuka kutokea kwa vitendo viovu ambavyo huchagizwa na mmomonyoko wa maadili na kuingia katika wimbi la uhalifu.

Aidha, Katabazi amekemea baadhi ya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wananchi hao vya kuwaficha wahalifu ambao wapo miongoni mwao kwa kuhofia kutoa taarifa za watoto wao huku akihimiza ushirikiano wa pamoja ili kuweza kuzuia na kutanzua uhalifu katika jamii.

Katika hatua nyengine Kamanda Katabazi ametembelea ujenzi wa kituo cha Polisi Kata ya Ihumwa kinacho jengwa Kwa nguvu ya wananchi na kupongeza Kwa hatua walizofikia na kuahidi kuunga mkono jitihada hizo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma pindi kitakapo kamilika.














Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA