Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Langoi akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Nyamwaga leo Januari 17, 2025.
Wanafunzi 5,080 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) hawajaripoti kuanza masomo kwenye shule zao.
Imeelezwa kwamba kati ya wanafunzi 6,313 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika halmashauri hiyo, ni 1,233 pekee waliokwisha kuripoti katika shule zao hadi sasa.
Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Langoi leo Januari 17, 2025 katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Nyamwaga kujadili na kupitisha bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2025/2026.
Langoi ameeleza kushtushwa na idadi ndogo ya wanafunzi walioripoti katika shule za sekondari na kuwataka madiwani na viongozi mbalimbali kuhamasisha wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
"Naomba waheshimiwa madiwani msaidie na ninyi kwa sababu hawa wanafunzi wanaishi sehemu mbalimbali ambapo mpo," amesema Langoi.
Ameongeza: "Hii ni aibu kwa halmshauri - kwa jambo kama hili. Waripoti shuleni haraka, angalau wiki ijayo takwimu iwe imepanda. Sisi ofisi kwa sehemu yetu tutachukuwa hatua."
Madiwani wakiwa kikaoni.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Petero Ntorogo amekazia wito kwa wazazi na walezi kuacha visingizio vya kutowapeleka watoto shule, akisema kuna changamoto yoyote watoe taarifa kwa mamlaka husika.
Ntogoro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwema amesema serikali haitasita kuchukua hatua kwa wazazi na walezi watakaokwamisha wanafunzi kwenda shule.
Katika kikao hicho, madiwani wamepitisha bajeti ya mapato na matumizi ya halmashauri hiyo kiasi cha shilingi bilioni 63.4, ambapo bilioni 41.5 ni kwa ajili ya kuendesha shughuli za kawaida, na bilioni 21.9 ni za miradi ya maendeleo.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akiwasilisha salamu za serikali kwenye kikao hicho amehimiza amani na mshikamano kwa viongozi katika kuwatumikia wananchi na kueleza miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Post a Comment