Na. Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma
Wananchi wa Wilaya ya urambo wameshauriwa kutumia maeneo ya hifadhi za Msitu za Mpanda Line wenye ukubwa wa Hekta 427,363.2, Msitu wa Hifadhi Ulyankulu wenye ukubwa wa Hekta 239,841.4 na Msitu wa Hifadhi wa vijiji vya Kangeme, Itebulanda na Utenge (KIU) wenye ukubwa wa ekari 860 kufanya shughuli za ufugaji wa Nyuki
Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) wakati akijibu swali la Mhe. Margareth Simwanza Sitta aliyetaka kujua Serikali itatenga lini eneo la sehemu ya Hifadhi ya Mto Ugalla ili Wananchi waweke mizinga ya asali.
Aidha Mhe. Kitandula alisema kuwa shughuli za ufugaji nyuki kwa wakazi wa Urambo na maeneo jirani kwa sasa zinafanyika katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Uyumbu yenye ukubwa wa kilomita za mraba 839 iliyopo Tarafa ya Usoke, Wilaya ya Urambo ambapo Wananchi kupitia vikundi mbalimbali vya ufugaji nyuki wameendelea kutumia eneo hilo mara baada ya Hifadhi ya Msitu Ugalla Kaskazini kupandishwa hadhi na kuwa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla.
Vilevile Naibu Waziri aliongeza kuwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 282 hairuhusu matumizi ya rasilimali zilizoko ndani ya maeneo ya hifadhi za Taifa badala yake Sheria hiyo inaruhusu uhifadhi wa wanyampori, utalii wa picha (non-consumptive utilization of resources) na tafiti za kisayansi.
Pia kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Taifa [kifungu cha 6(1)], mara eneo linapotangazwa kuwa hifadhi ya Taifa, haki, madai, upendeleo wowote uliokuwepo awali kuhusiana na chochote ndani ya eneo lililotangazwa kuwa hifadhi ya Taifa hukoma mara moja dhidi ya mtu yeyote isipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Kitandula alisema serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa ili kuendelea kujenga uelewa wa masuala ya uhifadhi wa maliasili hasa pale inapotokea eneo hilo linapandishwa hadhi.
Post a Comment