Watu saba wamepoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali mbaya iliyohusisha gari la kubebea wagonjwa (ambulance) na guta iliyokuwa imebeba watu 22.
Ajali hiyo imetokea leo asubuhi katika eneo la Mji wa Mafinga, barabara ya kuelekea Luganga, karibu na ofisi za Halmashauri ya Mji wa Mafinga.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo alipofika katika Hospitali ya Mji wa Mafinga, ambako majeruhi wanapatiwa matibabu.
Dkt. Salekwa amesema watu hao walikuwa wakielekea shambani kwa kutumia usafiri wa guta, ambao ni hatarishi kwa maisha yao, na kutoa wito kwa wananchi kuepuka kutumia vyombo visivyo salama kwa usafiri wa binadamu.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Mafinga, Dkt. Victor Msafiri, amesema wamepokea jumla ya majeruhi 15 pamoja na miili saba ya marehemu kufuatia ajali hiyo.
Amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 12 asubuhi, na hali za baadhi ya majeruhi ni mahututi huku wengine wakiendelea kupatiwa matibabu.
Mamlaka zinaendelea na uchunguzi kubaini chanzo kamili cha ajali hiyo.
Post a Comment