Wizara ya Afya imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya mkazi wa Daraja mbili mkoani Arusha Bi. Neema Kilugala aliyejifungua kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Arusha, Mount Meru.
Tukio hilo la tarehe 24 Machi, 2025 inaelezwa kuwa Bi. Neema anadai kuwa baada ya kujifungua alioneshwa mtoto wake na muuguzi akiwa ni mzima. Hata hivyo aligundua kuwa amebadilishiwa mtoto wake baada ya kuletewa mtoto akiwa amefungwa na vitenge ambavyo si vya kwake.
Muuguzi wa hosptali hiyo alidai kuwa alichanganya vitenge na vya mtoto mwingine hivyo akaahidi kwenda kubadilisha, pamoja na kuchukua hatua hiyo bado kulikuwa na hali ya sintofahamu. Kufuatia hali hiyo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha pamoja na Jeshi la Polisi imechukua hatua ya Kuchukua sampuli za wazazi waliojifungua kipindi hicho pamoja na za watoto kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Kumsimamisha kazi muuguzi aliyemhudumia ili kupisha uchunguzi.
Hata hivyo andiko hilo lililotolewa na Wizara ya Afya limeeleza kuwa baada ya uchunguzi kukamilika taarifa rasmi zitatolewa na hatua stahiki zitachukuliwa.
Post a Comment