Hali ya sintofahamu imeibuka baada ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kumsimamisha masomo Rais wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii, Victor Byemelwa, na kudaiwa kumwandikia barua Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, kumueleza kwamba wamemaliza kazi aliyowatuma.
Uongozi wa chuo hicho umethibitisha kumsimamisha masomo mwanafunzi huyo lakini ukikanusha kuandika barua kwenda kwa Kimbisa.
Jana kwenye mitandao ya kijamii, barua inayodaiwa kuandikwa Februari 5, mwaka huu na Mshauri wa Wanafunzi wa chuo hicho, Dick Manongi, ilikuwa ikisambazwa.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba Udom/Dos/36, ilikuwa na kichwa cha habari: "Ukamilisho wa kazi iliyopangwa kufanyika katika koleji ya Humanities & Social Science."
Iliendelea kusema: "Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi Udom, inapenda kukujulisha komredi Adam Kimbisa (Mwenyekiti wa CCM Dodoma,) kuwa kazi mliotupatia katika kutekeleza mkakati wa kuiondoa serikali ya wanafunzi wa upande wa Humanite, imekamilika kwa kijana Victor Byemelwa (aliyekuwa Rais) kuondolewa chuoni kwa kipindi kisichojulikana.
"Napenda kukuhakikishia kuwa kwa kuwa mashtaka yametolewa na Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Utawala na Fedha na yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, ni wazi kuwa kijana huyu hataweza kamwe kurudi chuoni hivi karibuni.
Tutumie sikukuu hii ya Chama kupanga mikakati ya kuweka serikali mpya tuitakayo mapema iwezekanavyo."
Akizungumzia sakata hilo, Manongi alikanusha kuandika barua hiyo na kudai kuwa imeghushiwa na tayari ameshatoa taarifa polisi katika kitengo cha ufuatiliaji makosa ya kimtandao (cybercrime) ili kutafuta aliyeighushi.
"Barua nimeiona, lakini naomba uwasiliane pia na uongozi wa chuo, mimi nisingependa kuzungumza hilo maana hilo suala nimelipeleka kwa watu wa Cyber Crime Dodoma, wao watatueleza hiyo barua imetoka wapi, binafsi sijaiandika," alisema Manongi.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano Udom, Beatrice Ntenga, alisema mwanafuniz huyo alisimamishwa kutokana na kosa la kuitisha Baraza la Shule bila kupata idhini ya Mkuu wa Chuo au Makamu Mkuu wa Chuo na kwamba amesimamishwa kwa muda usiojulikana.
Alisema mwanafunzi huyo anatakiwa kujibu mashtaka yake kwa mujibu wa taratibu za chuo na baadaye ataitwa kamati ya nidhamu.
"Barua hiyo tumeiona ikisambaa kwenye mitandao haijatolewa na Dean of Student, imeghushiwa maana muhuri na saini vinaonekana 'vimeskaniwa' na kuwekwa na hata hiyo kumbukumbu namba ya barua haipo kwa Dean ukiisogeza utagundua mapungufu mengi. Tumepeleka huko Cyber Crime wanafuatilia,"alisema Ntenga.
Alisema barua hiyo si ya kweli bali imetengezwa ili kutafuta huruma ya watu huku akithibitisha taarifa za barua hiyo zimewasilishwa polisi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kimbisa, alipopigiwa simu hakupokea na badala yake alitaka atumiwe ujumbe mfupi wa simu, baada ya kutumiwa ujumbe wa simu yake hakujibu.
إرسال تعليق