MABAO mawili ya winga mpya wa klabu ya Difaa Hassan El- Jadida yameipa Tanzania ushindi wa 2-0 dhidi ya Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Msuva aliyejiunga na timu ya Ligi Kuu ya Morocco mwezi uliopita leo alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya The Zebras na amefunga bao moja kila kipindi mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Elly Sasii aliyesaidiwa na Soud Lila na Frank wote wa Tanzania, hadi mapumziko Taifa Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Simon Msuva alipokea pasi ndefu ya kiungo Hamisi Abdallah wa Sony Sugar ya Kenya, akaikontroo vizuri na kumpasia kiungo wa Simba, Muzamil Yassin kabla ya kuiombea mbele na kuingia nayo kwenye boksi kwa kasi na kufumua shuti kali lililompita kama upepo kipa wa The Zebras, Mwambule Masule dakika ya sita.
Katika kipindi hicho, ilishuhudiwa Taifa Stars wakicheza vizuri zaidi na kutengeneza nafasi chache za kufunga, ambazo hata hivyo walimudu kuitumia vizuri moja tu kupata bao.
Mashambulizi ya Taifa Stars leo ambayo katika benchi la Ufundi imeongezewa nguvu na mchezaji wa zamani, Amy Ninje aliyecheza hadi Uingereza Ligi za Madaraja ya chini na kocha wa zamani wa Azam, Dennis Kitambi ambaye kwa sasa anafundisha AFC Leopards ya Kenya.
The Zebras nao hawakuwa wanyonge kabisa uwanjani, kwani walipeleka mashambulizi langoni mwa Taifa Stars na kukaribia kufunga mara mbili kama su uhodari wa kipa wa Simba, Aishi Salum Manula.
Kipindi cha pili, Zebras walirudi kwa nguvu na kuanza kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Taifa Stars, lakini safu ya ulinzi ikiongozwa na mkongwe Kevin Yondan ilikuwa imara kudhibiti hatari zote.
Hatimaye Msuva akawainua tena vitini mashabiki wa nyumbani kwa kufunga bao la pili dakika ya 63 baada ya kugongeana vizuri na winga wa Simba SC, Shiza Ramadhani Kichuya.
Nahodha, Mbwana Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji alicheza vizuri pamoja na kudhibitiwa vikali na akakaribia kufunga mara mbili – unaweza kusema bahati haikuwa ya kwake leo.
Kiungo wa Tenerife ya Hispania, Farid Mussa na mshambuliaji wa Dhofar ya Oman wote waliingia kipindi cha pili na wakacheza vizuri sawa na chipukizi, Emmanuel Martin wa Yanga aliyempokea Msuva.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kevin Yondan, Himid Mao, Simon Msuva/Emmanuel Martin dk82, Hamisi Abdallah/Said Ndemla dk80, Muzamil Yassin/Raphael Daudi dk57, Mbwana Samatta/Elias Maguri dk82 na Shiza Kichuya/Farid Mussa dk66.
Botswana; Mwambule Masule, Mosha Gaolaolwe/Jackson Lesole dk74, Edwin Olerile/Tmisang Orebonye7 dk4, Simisami Mathumo, Lopang Mogise, Alphonce Modisaotsile, Maano Ditshupo/Katlego Masole dk70, Gift Moyo, Segolame Boy, Kabelo Seakanyeng na Ontireste Ramatlhakwana.
إرسال تعليق