UONGO #1: Serikali imekodisha Bandari ya Dar es Salaam kwa DP World kwa miaka 100
Ukweli: Hakuna mkataba wowote wa ukodishaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambao umesainiwa hadi sasa. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Iko kwenye MAJADILIANO na DP World kuhusu uendelezaji wa bandari nchini
Hakuna kipengele chochote kwenye makubaliano yoyote ya awali kati ya DP World na Tanzania kinachotaja ukodishaji wa miaka 100
UONGO #2: Serikali imeuza bandari ya Dar es Salaam kwa mwekezaji wa nje
Ukweli: Hakuna uwezekano wowote wa Serikali kuuza bandari yoyote nchini. Kinachopangwa kufanyika ni UKODISHAJI wa sehemu ya bandari ili kuongeza idadi ya shehena, ufanisi na mapato ya kodi
UONGO #3: Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kubinafsisha bandari
Ukweli: Kumekuwa na UWEKEZAJI binafsi katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia kampuni ya TICTS kwa takribani miaka 30, kuanzia zama za marais Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, John Magufuli hadi sasa.
UONGO #4: Kampuni ya DP World haina uwezo wowote ule na ni wababaishaji
Ukweli: Kampuni ya DP World inamilikiwa na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). DP World ni moja ya kampuni kubwa na zinazoheshimika duniani, ambayo inaendesha bandari kwenye nchi karibu 50 duniani, ikiwemo mataifa 10 ya Afrika
DP World inaaminiwa kuendesha bandari kwenye mataifa makubwa kabisa duniani, ikiwemo Marekani, China, Ujerumani, Ufaransa na Canada. Kwa upande wa Afrika, wapo Nigeria, Afrika Kusini, Rwanda, Misri, Msumbiji na nchi nyingine
Kwa mwaka 2022 peke yake, DP World ilipata mapato ya Dola za Marekani Bilioni 17.1 na faida ya Dola Bilioni 5 (sawa na shilingi trilioni 12).
DP World imewekeza zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 1.8 kwenye bara la Afrika katika miaka kumi iliyopita na inapanga kuwekeza Dola za Marekani Bilioni 3 (shilingi trilioni 7.2) kwenye bara hili katika miaka ijayo.
UONGO #5: Tanzania haiwezi kupata faida yoyote kutokana na uwekezaji binafsi kwenye bandari ya Dar es Salaam
Ukweli: Uwekezaji binafsi ni jambo la kawaida kwenye bandari nyingi kubwa Afrika, Marekani, Asia na sehemu nyingine duniani.
Tanzania inatarajia kupata manufaa yatuatayo kutokana na uwekezaji binafsi kwenye bandari ya Dar es Salaam:
(a) kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na uwekezaji mkubwa na ongezeko la Shehena ya Mizigo itakayopitia Bandari ya Dar es Salaam;
(b) kuongezeka kwa ufanisi katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi na kuleta tija stahiki katika mnyororo wa thamani wa huduma za bandari nchini;
(c) kuongezeka kwa pato la Taifa kutokana na uboreshaji wa shughuli za kibandari;
(d) kuongeza tija na kuwezesha mwendelezo wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imekuwa ikijengwa na Serikali kama vile Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa meli za mizigo katika Maziwa Makuu, na Mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam; na
(e) kuchagiza na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi (Multiplier Effect)
zikiwemo Kilimo, Utalii, Viwanda, Mifugo, Uvuvi, Biashara na Usafirishaji na hivyo kuboresha ustawi wa Watanzania kwa ujumla.
إرسال تعليق