Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Vyombo Vingine vya Ulinzi na Usalama wakiwemo JKT Ruvu imefanya operesheni ya siku nane (8) mfululizo mkoani Morogoro katika wilaya za Morogoro, Morogoro vijijini na Mvomero na kukamata jumla ya gunia 131 za bangi kavu iliyo tayari kusafirishwa, kilo 120 za mbegu za bangi na kuteketeza jumla ya hekari 489 ya mashamba ya bangi ambapo jumla ya watuhumiwa 18 wanashikiliwa kuhusika na dawa hizo.
Katika wilaya ya Morogoro vijijini kata ya Kisaki, kijiji cha Rumba zimekamatwa gunia 70 za bangi, Kijiji cha Mbakana zimekamatwa gunia 59 za bangi, kilo 120 za mbegu za bangi na kuteketezwa hekari 350 za mashamba ya bangi.
Aidha, wilayani Mvomero Mamlaka imeteketeza hekari 139 na wilaya ya Morogoro zimekamatwa gunia mbili (2) za bangi.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, kamishna jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, wakulima wa bangi mkoani Morogoro wanalima pembezoni mwa mto, na kukata miti ili wawezekupata maeneo ya kulima bangi.
“Wakulima wa bangi wa mkoa huu wanachepusha maji na kuyazuia yasiende kwenye maeneo mengine yakahudumie wananchi ili kumwagilia mashamba yao. Pia wanafanya uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata miti katikati ya msitu ili waweze kulima bangi. Hivyo, wanafanya uharibifu mkubwa wa mazingira na kuharibu vyanzo vya maji katika maeneo haya” ,amesema kamishna jenerali Lyimo.
Pia, amesema kwamba, wakulima wa bangi wanalima mashamba yao katika maeneo ya mbali, yaliyojificha na yasiyoweza kufikika kirahisi lakini Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeweza kuyafikia maeneo hayo kuwakamata wanaojihusisha na bangi, pamoja na kuteketeza bangi iliyovunwa na mashamba yao.
“Kwa mfano katika maeneo haya ya Morogoro ambayo tumefanya hii operesheni, eneo ambalo wamelima bangi ni mbali kutoka mjini. Kutoka unapoachia gari mpaka kufika huku unatembea masaa sita mwendo wa kijeshi. Kwa hiyo wanaamini hakuna mtu anayeweza kufika” ,ameongeza kamishna jenerali Lyimo.
Aidha, amewaasa waanchi kutoa taarifa juu ya watu wanaolima bangi na mirungi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Niwaase wananchi wote Tanzania watusaidie kutoa taarifa za wakulima wa bangi na mirungi katika maeneo mbalimbali ili tuwakamate na kuharibu mashamba yao. Kwani mbali na madhara mengine yanayotokana na zao la bangi, wakulima hawa wanaharibu misitu, vyanzo vya maji, na wanaweza kutengeneza jangwa kwani wanakata miti sana ili wapate maeneo ya kulima bangi”,amesema.
Kulingana na Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2022, mkoa wa Morogoro ni kati ya mikoa mitano iliyokithiri kwa kilimo cha bangi Nchini Tanzania.
إرسال تعليق