BARRICK NORTH MARA YAANZA FIDIA WANANCHI WA NYAHETO KUPISHA UPANUZI WA MGODI


Lori likiwa kazini katika mgodi wa North Mara
***

Zoezi la kulipa fidia kwa wananchi katika eneo la Nyeheto wilayani Tarime, Mara linaendelea vizuri na wengi wanaripotiwa kujitokeza kupokea malipo yao.

Wananchi hao wanalipwa fidia hiyo ili kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals. Kampuni ya Barrick imetenga shilingi zaidi ya bilioni 5.6 kulipa fidia kwa wananchi 1,808 katika eneo hilo.

Taarifa kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara zinaonyesha kuwa hadi kufikia Jumanne iliyopita, wananchi zaidi ya 600 walikuwa wamejitokeza kuchua malipo yao ya fidia.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, hatua hiyo ya malipo ya fidia imekuja baada ya mgogoro uliokuwepo baina ya wananchi hao kupata suluhisho.

Mntenjele anaendelea kutoa wito wa kuhamasisha wananchi hao kuchangamkia malipo hayo ya fidia ili kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi huo.

“Wachukue malipo yao ya fidia haraka ili waondoke kupisha uwekezaji wa mgodi huo,” DC Mntenjele alisisitiza katika wakati wa mahojiano na vyombo vya habari karibuni.

Alisema serikali inashirikiana na mgodi wa Barrick North Mara vizuri - hata katika jitihada za kuboresha mahusiano na jamii inayouzunguka.

Alifafanua kuwa jitihada hizo zinahusisha utoaji wa elimu juu ya faida za mgodi huo, sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi katika vijiji vinavyopakana nao.

“Suala la mahusiano ya mgodi wa Barrick North Mara na jamii inayouzunguka liko vizuri,” alisema DC Mntenjele na kuongeza kuwa mgodi huo pia umekuwa ukiandaa mashindano ya soka ya Mahusiano Cup ili kuboresha uhusiano kati yake na jamii inayouzunguka.

Alitaja mradi wa kilimo biashara cha mbogamboga unaoendeshwa na vijana katika kijiji cha Matongo, akisema ulianzishwa kwa ufadhili wa mgodi wa Barrick North Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kama sehemu ya kuboresha mahusiano, lakini pia kuwezesha vijana hao kuwa na shughuli mbadala ya kujipatia kipato.

“Kupitia elimu tunayotoa pamoja na miradi ya kijamii inayofadhiliwa na Barrick katika vijiji husika, ukiwemo huo wa kilimo biashara, vijana watashawishika kuachana na vitendo vya kuvamia mgodi huo,” alisema.


Vile vile katika juhudi za kuboresha mahusiano, mgodi wa Barrick North Mara umekuwa ukikarabati barabara muhimu za vijiji jirani mara kwa mara ili kurahisisha usafiri wa wananchi.


Kwa upande mwingine, kampuni mbalimbali za wazawa zinafanya kazi na mgodi huo, fursa ambayo pia inachangia kuzalisha ajira kwa vijana, na hivyo kuongeza mzunguko wa fedha katika vijiji jirani.

Kampuni ya Barrick pia imekuwa ikitoa misaada ya vifaa tiba na kukarabati miundombinu ya kituo cha afya Nyangoto “Sungusungu” kilichopo katika mji wa Nyamongo, kilomita chache kutoka mgodi wa North Mara, miongoni mwa misaada mingine ya kijamii ndani ya vijiji vinavyopakana nao.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA