BENKI YA CRDB KUENDELEA KURAHISISHA UKUSANYAJI MAPATO HOSPITALI YA KCMC

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.


Benki ya CRDB na Hospitali ya Kanda ya KCMC iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, zimeingia makubaliano ya kuendelea kuifanya Benki ya CRDB kuwa mtoaji wa huduma za fedha hasa ukusanyaji mapato hospitalini hapo.

Azma ya Benki ya CRDB siku zote ni kuhakikisha inatoa huduma bora na shindani zinazokidhi mahitaji ya wateja wake ikiamini kuwa huduma bora, za kisasa, jumuishi na rahisi za fedha ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Hivyo, Benki ya CRDB imewekeza rasilimali zake katika ubunifu wa huduma na bidhaa zake, ikiwamo kuanzisha na kuboresha kiendelevu mfumo wa upokeaji na ufanyaji malipo kwa njia za kieletroniki unaotumika kwenye taasisi tofauti ikiwemo hii ya Hospitali ya KCMC.
Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema Hospitali ya KCMC ni moja ya taasisi za mwanzo kuingia ubia na Benki ya CRDB kutumia mfumo huu wa malipo, mwaka 2014. Ubia huu ulienda sambamba na uzinduzi wa kadi maalum ya malipo ya Hospitali ya KCMC iliyopewa jina “TemboCard KCMC.”

Katika mwaka wa kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo hospitalini hapo, zaidi ya shilingi bilioni 4.1 zilikusanywa na mpaka mwaka 2022, makusanyo hayo yameongezeka mara mbili na kufika shilingi bilioni 8.7 kwa mwaka.

“Tangu tulipoingia mkataba na Hospitali ya KCMC kuanza kuutumia mfumo wetu mpaka mwaka jana, tumeiwezesha Hospitali ya KCMC kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 52.8. Hiki ni kiasi kikubwa kukusanywa ndani ya miaka minane na makusanyo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka,” amesema Raballa.
Raballa amesema katika kuimarisha ushirikiano na hospitali na pia ili kusogeza karibu zaidi huduma kwa wateja wake mwaka 2020 Benki ya CRDB ilifungua tawi hospitaini hapo. Tawi hilo linawafaa pia wafanyakazi wa hospitali, wanafunzi wanaojifunza hospitalini hapa, wagonjwa, wafanyabiashra na wananchi kwa ujumla wanaoishi au kupita maeneo ya hospitali.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema kabla hawajaanza kutumia mfumo wa Benki ya CRDB, walikuwa wanakusanya mapato kidogo na kuna nyakati walilipwa hata kwa fedha bandia .

“Kama mnavyofahamu uendeshaji wa hospitali ni wa gharama kubwa, hivyo usimamizi wa mapato ni kati ya vipaumbele muhimu vya hospitali yoyote. Ndio maana leo tupo tena hapa kuuhuisha mkataba wetu ili kuendelea kuwa na ufanisi mkubwa katika ukusanyaji wa mapato yetu,” amesema Profesa Masenga.
Awali, mkurugenzi huyo amesema wahasibu walilazimika kukaa na fedha nyingi kwenye ofisi zao jambo lililokuwa linawaweka kwenye hatari ya kuvamiwa hivyo kupoteza mapato ya hospitali ndio maana mwaka 2004 ilikuwa rahisi kwa menejimenti ya hospitali kushawishika kuingia makubaliano na Benki ya CRDB kutumia teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato na kwamba mfumo huu umeondoa makosa ya kibinadamu kwa kiasi kikubwa hivyo kuongeza makusanyo.

Profesa Masenga pia amesema uhusiano wa Benki ya CRDB na Hospitali ya KCMC hauishii kwenye huduma za benki pekee kwani wao ni miongoni mwa wanufaika wa uwekezaji unaofanywa kwa jamii na Benki ya CRDB.
Profesa Masenga amesema Benki ya CRDB imewajengea eneo la mapumziko kwa wagonjwa na wasaidizi wao, na mara kadhaa imewasaidia vifaatiba na kompyuta ili kuboresha utoaji wa huduma hospitalini.

Kutokana na makubaliana haya, sio hospitali pekee itakayonufaika na mfumo huu bali pia wale wote wanaohudumiwa hospitalini hapa. Malipo sasa yatakuwa yanafanyika kutumia ‘control number’ . Hivyo yeyote anayehudumiwa Hospitali ya KCMC hata hitaji kufanya malipo kwa fedha taslimu, hivyo kuweza kufanya malipo kielektroniki.

Mhudumiwa ataweza kulipa kwa kutumia kadi za benki ikiwemo za Visa na MasterCard, pia ataweza kutumia SimBanking, internet banking na pia CRDB wakala. Malipo haya ya kisasa yanamwezesha mfanya malipo yoyote kulipia huduma ya kwake au ya mtu mwingine moja kwa moja hospitalini, akiwa popote alipo, ndani au nje ya nchi ilimradi awe na control number, ulipo tupo!
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA