HAKI HUINUA TAIFA, SITALIPIZA KISASI- MAKONDA

 

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi CDE. Paul Makonda amewatoa hofu wale wote wanaodhani atatumia nafasi hiyo kulipiza kisasi kwa kile walichohisi hakikuwa sawa na badala yake atatekeleza jukumu lake kulingana na maagizo ya chama kwa maslahi ya Taifa.


Ameyasema hayo leo Oktoba 26, 2023 wakati akihutubia katika hafla ya mapokezi iliyofanyika Ofisi ndogo za Chama Cha Mapinduzi CCM , Lumumba Jjiini Dar es Salaam huku akeleza kutokuwa na kisasi na yeyote.

"Wengi wao wanawaza kwamba Makonda ataenda kulipa kisasi, wanawaza makonda atakwenda kufanya nini, wengine wanasema Usiyemtaka kaja na alikuwa haonekani alienda kujificha wapi? nasema mbele ya watanzania na Mbele ya Mwenyenzi Mungu mimi sina kisasi kwa mtu yeyote." Amesema Makonda


"Wale wote mnaofikiri ya kwamba kuna jambo halikuwa sawa mimi naelewa kwamba Mungu aliwatumia kunisaidia kumjua Mungu zaidi msiwe na hofu kwangu ninyi wote ni watumishi wa Mungu, Dkt. Samia hajaniteuwa kuja kuhangaika na mambo ya Makonda bali kuhangaika na itikadi uenezi wa Chama cha Mapinduzi na wala kamati kuu haikukaa kumtafuta mtu wa kulipiza kisasi" Amesema Makonda

 

Ameongeza kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mheshimiwa Dkt. Samia na Kamati Kuu walikaa kutafuta mtu atakae ongeza nguvu katika kujenga imani ya Watanzania kwenye Chama Cha Mapinduzi kwani huu siyo muda wa kuweka mambo binafsi bali ni kuwatumikia Watanzania.


Ametumia nafasi hiyo kutuma salamu kwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na watendaji  wote wa serikali  Nchini kutekeleza majukumu yao kikamilifu na endapo ikibainika kuto tekeleza vyema Chama hakitasita kuwachukulia hatua kwani Chama Cha Mapinduzi ni sikio la Serikali na  sauti ya wananchi.


"Pale patakapo bainika hamjafanya kazi yenu kikamilifu Chama hakitasita kuwachukulia hatua, sipo tayari kuwa msemaji wa Chama ambacho kimepewa dhamana na wananchi na wanaomsaidia Mhesimiwa Mwenyekiti wanashindwa kutekeleza nisimame hadharani kusema uongo, Hapana! Kila kiongozii wa Serikali atabeba msalaba wake mwenyewe, Haki huinua Taifa" Amesema Makonda


Awali akikabidhiwa ofisi ameomba ushirikiano kwa watendaji wote ikiwa ni pamoja na kupewa taarifa sahihi kwa maamuzi sahihi kwa kukijenga chama kwa wananchi huku akiahidi kuendelea kuwasaidia akina mama wajane na kumwomba Ndugu Sophia Mjema ambaye kwa sasa ni Mshauri wa  Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum kuwaweka Wajane kama Kundi maalum.


Kwa upande wake aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi ambaye kwa sasa ni Mshauri wa  Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum Ndugu Sophia Mjema amemtaka Makonda kusimamia majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi Kinaendelea kushinda.


"Nakutakia kila lakheri  katika kazi hii kwasababu ndio Moyo wa Chama Cha Mapinduzi kinakutegemea sana, endelea kuendeleza idara hii" Amesema Mjema


Ikumbukwe kuwa Mnamo Oktoba 22, 2023 Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ilimteua Ndugu Paul Makonda kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi akichukua nafasi ya Ndugu Sophia Mjema ambaye aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mshauri wa  Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum kuwaweka Wajane kama Kundi maalum.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA