Sera ya Mitaala Mipya ya Elimu ikipitishwa inatarajiwa kuanza kutekelezwa Januari 2024 kama mapendekezo yaliyopo hayatabadilishwa ambapo miongoni mwa mapendekezo hayo ni ya mkondo wa mafunzo ya amali ambayo yatamsaidia mhitimu kujiajiri na kuajiriwa.
Kauli hiyo imetolewa leo Oct 10 mwaka 2023 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolfu Mkeda katika Mkutano wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Wamiliki wa Shule Zisizo za Serikali wenye lengo la kusikiliza, kufahamu na kutatua changamoto zilizomo kwa kushirikiana na kutoka na Azimio moja.
Profesa Mkenda amewataka wamiliki hao wa shule binafsi kuwekeza katika Mkondo wa shule za Mafunzo ya Amali kwani mafunzo hayo yanahitaji uwezeshaji toshelevu na kama kuna sehemu watahitaji serikali iwasaidie watoe maoni yao na serikali ipo tayari kuwasikiliza.
"Nawaomba muwekeze semeni Serikali tufanye nini ili nyie muweze kuwekeza mtufungulie njia, Tushikane mkono tunawahitaji sana sekta binafsi muwekeze katika mkondo wa mafunzo ya amali, serikali chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan tuone tunaweza tuka'facilitate' (wezesha) vipi ambao mtapenda kuwekeza katika mkondo huo." Amesema Prof. Mkenda
Kutokana na maswali mengi ya wadau kwamba ni kwanamna gani waalimu wataendana na Mitaala Mipya Waziri Profesa Mkenda amewatoa wasiwasi kuwa waalimu wataandaliwa ili kuendana na Mageuzi katika sekta hiyo.
Baada ya muhitimu kupata elimu atahitaji kutumia elimu aliyonayo kujiajiri au kuajiriwa kwa mantiki hiyo Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu Ajira , Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu inalo jukumu la kuratibu, kusimamia na kuwezesha na kwa kuzingatia hilo Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Patrobas Paschal Katambi amewasisitiza kutoa elimu bora inayoendana na misingi ya Maadili kwa mustakabali wa Taifa na Vizazi vijavyo.
"Tunapaswa kushirikiana kuhakikisha tunakuwa na Sera bora, sheria na utekelezaji mzuri wa majukumu ili serikali itimize wajibu wake wa kutengeneza mazingira wezeshi kwa vijana hasa katika sekta ya elimu kwani ndiko tunapopata taifa endelevu ili kupata wafanyabiashara bora, na kama ni viongozi watakuwa bora sana kwasababu watakuwa wamejengwa vizuri katika misingi ya elimu"Amesema Prof. Katambi
Aidha katika sekta ya makuzi na malezi ya vijana amesema jukumu kubwa ni kuwatambua kuwasikiliza na kuwasaidia kwa kuwafanya wawe na mtazamo chanya, ndoto, shabaha, Malengo na Matamanio ya kutoa mchango gani wa uzalendo kwa taifa.
Hata hivyo Mkutano huo unaenda sambamba na kauli mbiu isemayo "Ushirikishwaji wa Wadau Kwa Elimu Bora".
إرسال تعليق