Na Lilian Lundo na Zuena Msuya
Mhe. Kapinga amesema hayo leo Oktoba 8, 2023 wakati wa hafla ya uwashaji umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Kijiji cha Litumbandyosi, kilichopo Kata ya Litumbandyosi, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
“Mhe. Rais ametoa fedha mpate umeme, mtapata umeme. Niwahikikishie ndugu zangu wa Kingoli umeme unakuja, tutamsimamia Mkandarasi kuhakikisha nguzo zinakuja na umeme unawasha, ili na nyie pia mpate umeme. Hatutawaangusha, tutahakikisha mnapata umeme,” amesema Mhe. Kapinga.
Ameendelea kusema kuwa, Mhe. Rais ametoa fedha kwa vijiji vyote vya Tanzania ambavyo bado havijapata umeme vipate umeme ikiwemo vijiji Vinne vya Litumbandyosi vilivyopo wilayani humo.
Aidha, Mhe. Kapinga amemtaka Mkandarasi ambaye anatekeleza mradi wa kufikisha umeme Wilaya ya Mbinga kuhakikisha Vijiji 45 vya Mbinga Vijijini na Vijiji 14 vya Mbinga Mjini ambavyo bado havijavifiwa na umeme vinafikiwa na umeme kabla ya Desemba 30, 2023.
Vilevile amesema kuwa Serikali itapeleka umeme katika maeneo yote yenye shughuli za kijamii na kiuchumi kupitia mradi wa kupeleka umeme kwenye huduma za kijamii, zikiwemo shule, vituo vya afya, misikiti, makanisa na visima vya maji.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Yusuph Ismail ambaye pia ni Meneja Uthibiti na Ufuatiliaji wa Miradi REA amesema Wilaya ya Mbinga imepewa shilingi bilioni 28.8 kwa ajili ya kupeleka umeme vijiji ambavyo bado havijavikiwa na umeme.
Amesema kuwa katika fedha hizo Wilaya ya Mbinga Vijijini imepata shilingi bilioni 19.8 na Mbinga Vijijini imepata shilingi bilioni 9, “ Kwa upande wa Mbinga Vijijini, Mkandarasi anatarajia kupeleka umeme vijiji 45 vilivyobaki kufikia Desemba 30, 2023” amesema Mhandisi Ismail.
Amesema mpaka kufikia mwisho wa mwezi Oktoba Mkandarasi atakuwa amefikisha umeme vijiji 20, na mwishoni mwa mwezi Novemba atakuwa amefikisha umeme katika vijiji vingine 21 na Vijiji 4 vitafikishiwa umeme mwezi Desemba mwaka huu.
إرسال تعليق