Na MWANDISHI WETU, MWANZA
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Mhe. Elikana Balandya ameupongeza Mfuko wa Taifa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuanzisha Mfumo wa kusajili waajiri na wanachama kwa njia ya mtandao jambo ambalo limewapunguzia waajiri na wanachama muda na gharama za kusafiri kwenda kwenye ofisi za NSSF kufuata huduma.
Akizungumza jijini Mwanza katika Ofisi za NSSF, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Amos Makalla, wakati wa kufunga maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja yenye kauli mbiu isemayo ‘Team Service’ na kauli mbiu ya NSSF ni ‘Ushirikiano kwa Huduma Bora’, amesema kupitia mfumo huo, NSSF imetekeleza kwa vitendo maagizo ya Serikali Mtandao.
“Nimefurahishwa na suala la kuanzisha mfumo wa kusajili waajiri na wanachama kimtandao yaani lango la mwajiri (employer portal) na lango la mwanachama (member portal). Mifumo hii inapunguza muda na gharama za kufuata huduma kwenye ofisi za NSSF,” amesema Mhe. Balandya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amemshukuru Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa uongozi wake umeweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji hapa nchini, hali ambayo imechangia kuongezeka kwa miradi inayotekelezwa kwa ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi.
Akizungumzia utendaji wa NSSF, Mshomba amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, Mfuko umekua hadi kufikia Trilioni 7.572 ukilinganisha na mwaka 2021/22 ambapo ulikua na thamani ya trilioni 6.079.
“Ukuaji huu wa Mfuko umetokana na kuongezeka kwa wanachama ambapo tulifanikiwa kusajili wanachama wapya 226,772 kati yao, wanachama 198,998 ni kutoka sekta rasmi na 44,897 kutoka sekta isiyo rasmi,” amesema Mshomba.
Amesema Mfuko ulikusanya michango yenye thamani ya shilingi trilioni 1.716 katika mwaka 2022/23, mapato yatokanayo na uwekezaji pia yameendelea kuongezeka ambapo katika mwaka wa fedha 2022/23, Mfuko ulipata mapato yenye thamani ya shilingi bilioni 7.153 sawa na asilimia 55 ukilinganisha na mapato yenye thamani ya shilingi bilioni 4.622.25 yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2022/23
Kuhusu ulipaji wa mafao, Mshomba amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Juni 2023, Mfuko ulilipa mafao yenye thamani ya shilingi bilioni 745.72 ikiwa ni ongezeko la asilimia 13 ukilinganisha na mafao ya shilingi bilioni 659.77 yaliyolipwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022.
Mshomba amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na maboresho ya huduma katika maeneo mbalimbali ikiwemo lango la elektroniki la huduma kwa waajiri na wananchama, kuboresha eneo la ukaguzi kwa waajiri ambapo kaguzi hizo kwa sasa hufanyika kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (inspection portal), kuendesha semina kwa waajiri na wanachama, kuanzisha mifumo ya ushirikiano na Taasisi zingine za Serikali na kuboresha mifumo ya kielektroniki.
إرسال تعليق