Mgeni rasmi Dkt. Phumzile Mlambo - Ngcuka (aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UN Women na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
Na Holiness Ulomi - Dar es salaam
Wanaharakati wa haki za wanawake zaidi ya 2000 wakiwemo wawakilishi wa Asasi za kiraia kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki katika Tamasha la 15 la Jinsia ambalo linafanyika kuanzia Novemba 7,2023 mpaka Novemba 10,2023 katika Viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Jijini Dar es salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Tamasha hilo leo Mgeni rasmi alikuwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UN Women na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Dkt. Phumzile Mlambo Ngcuka ameipongeza TGNP kwa harakati mbalimbali inazozifanya katika kupigania usawa wa kijinsia na kupinga ukatili wa kijinsia ikiwemo ndoa za utotoni na ukeketaji.
Dkt. Phumzile ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wanaume kushiriki kwa nguvu zote katika kutetea usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha wanapigania usawa wa ajira na mishahara kwa wanawake na wanaume, kubomoa mifumo dume, kupinga ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia.
"Wanaume wasiachwe nyuma katika uanaharakati wa kimapinduzi. Kizazi hiki kinahitaji wanaume wenye harakati za kudumisha usawa kati ya mwanamke na mwanaume kwenye jamii, ifike wakati wanaume waseme mishahara tunayopewa kazini iwe sawa na kama mwanamke anapewa mshahara mdogo aseme haiwezekani, basi mwanaume huyo aamue kuacha kazi",amesema Dkt. Dkt. Phumzile
"Pia ifike wakati wanaume wagome kabisa kuwaoa mabinti wenye umri mdogo na kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza ndoa za utotoni. Lakini pia tuhakikishe usawa wa kijinsia unaanzia majumbani mwetu, harakati zianzie ngazi ya chini kabisa kwenye famili",ameongeza Dkt. Phumzile.
إرسال تعليق