KIKUNDI CHA WOMEN FORCE KIMETOA MSAADA WA VITI VYA WAGONJWA HOSPITALI YA MANISPAA SHINYANGA


Mwenyekiti wa kikundi cha Women Force Nsianel Gerald akikabidhi viti vya kubebea wagonjwa kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mussa Makungu.
Picha ya pamoja.

Na Mwandishi wetu- Malunde 1 blog

Kikundi cha Women Force kilichopo mkoani Shinyanga kimetoa msaada wa viti vya kubebea wagonjwa katika hospitali ya manispaa ya Shinyanga.

Zoezi hilo la utoaji wa viti vya wagonjwa limefanyika leo Novemba 10, 2023 katika jengo la wagonjwa wa nje kwenye hospitali ya Manispaa ya Shinyanga vyenye thamani ya shilingi milioni 2.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo,  Mwenyekiti wa kikundi cha Women Force Nsianel Gerald ameeleza malengo ya kikundi hicho kuwa ni kusaidiana na kuinuana kiuchumi pamoja na kutoa msaada kwenye jamii ambapo wamekuwa na utaratibu wa kufanya hivyo kila mwaka na kutoa hamasa kwa vikundi vingine kushiriki shughuli za kijamii.

“Moja ya maazimio ya kikundi chetu ni kila mwaka kuisaidia jamii kwa kutoa msaada kwa kile tulichobarikiwa na sisi tunarudisha kwenye jamii inayotuzunguka, lakini pia ni matarajio yetu kama kikundi cha Women Force kuisaidia jamii kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya kama hivi leo tumeweza kutoa msaada wa viti vitano vya wagonjwa katika hospitali hii ya Manispaa ya  Shinyanga, pia tunahamasisha na wadau wengine kujitolea sababu uhitaji bado ni mkubwa kwenye maeneo mbalimbali waendelee kujitoa kuisaidia jamii”, amesema Nsianel Gerald.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mussa Makungu mara baada ya kupokea vifaa hivyo amewapongeza wanakikundi cha Women Force kwa hatua walizochukua kutoa msaada kwenye hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na kutambua uhitaji uliopo kwenye hospitali hiyo.

“Nipende kuwapongeza kwa sababu ni vikundi vichache vinavyoweza kufanya jambo kama hili, hasa kwenye maeneo ya utoaji wa huduma kama hospitali sisi kama serikali tunatambua mchango wa wadau muhimu kwa kuweza kuchangia kwenye maendelea ndani ya jamii, niwaombe msichoke kuendelea kujitolea kulingana na uhitaji uliopo, si hapa tu kunamaeneo mengi yenye uhitaji ikiwemo vituo vya afya na zahanati, tunawashukuru sana kwa msaada huu mliotupatia”, amesema Mussa Makungu.

Mwenyekiti wa kikundi cha Women Force Nsianel Gerald akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mussa Makungu akizungumza wakati wa makabidhiano hayo.
Mganga Mkuu Manispaa ya Shinyanga Dkt.  Elisha Robert (kulia) wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo.


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA