SERIKALI YAWATAKA WAHITIMU WA MISITU KUWA WAADILIFU KATIKA USIMAMIZI WA HIFADHI NA MISITU NCHINI


Serikali kupitia  Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka wahitimu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi kutumia elimu waliyoipata kuwa waadilifu, wazalendo, kusimamia uhifadhi pamoja na matumizi endelevu ya misitu.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 17 Novemba, 2023 na Mkurugenzi wa Mafunzo  na Utafiti, Dkt. Edward Kohi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas wakati wa mahafali ya 26 ya Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi ambapo ametunuku wanafunzi 200 ikiwemo 124 wa Astashahada na 76 wa Stashahada za Teknolojia ya Viwanda vya Misitu za Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi.

" Nawaasa Wahitimu mnaohitimu leo kutumia elimu mliyoipata kuwa waadilifu, wazalendo na kuheshimu dhamana mtakayopewa katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu."  amesema 
Dkt. Kohi ameongeza kuwa " Wahitimu wana mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa misitu na mazingira zinazoongezeka kwa kasi hapa nchini, Ni wajibu wenu kutumia elimu na mbinu mlizozipata na kuwa wabunifu katika kutoa huduma kwa wananchi kwa bidii na haki."

Amesema wahitimu wa fani ya teknolojia ya viwanda vya misitu ni hazina kubwa kwa Taifa ikizingatiwa kuwa ndiyo wanaohitajika zaidi kwa matumizi endelevu ya maliasili za misitu nchini kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

"Mafunzo haya ni muhimu sana katika jitihada za Serikali za kukuza uchumi na kuondoa umaskini."amesema 

Amesema taifa linahitaji wahitimu wenye ujuzi wakutosha na nidhamu kwa matumizi endelevu ya  misitu na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo yenye ubora katika sekta ya misitu na nyuki ili kujenga uchumi imara na kukuza ajira kwa vijana. 

Amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kuimarisha mfumo mzuri wa kuwapatia nafasi za kazi vijana wetu kila fursa zitakapopatikana. 
Aidha, ameutaka Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuendelea kukisaidia Chuo hicho ili kujenga uzoefu na kutumia wanafunzi wa chuo hiki katika kazi za kuendeleza na kuhamasisha matumizi endelevu ya misitu nchini.

Sambamba na hayo, Dkt. Kohi alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Finland kupitia Mradi wa Panda Miti Kibiashara kuwezesha ukamilishaji wa mitaala ya mafunzo ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu kwa ngazi ya VET.

Pia kuwezesha programu ya ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Finland (HAMK) na vyuo vya FITI-Moshi na FTI-Olmotonyi katika kubadilishana uzoefu wa namna bora ya ufundishaji wa mafunzo kwa vitendo na matumizi ya mafunzo kwa mtandao. 

Aidha, Dkt. Kohi alielekeza uongozi wa Chuo hicho kuhakikisha wanajitangaza zaidi ili kupata wadau wengi wa kujiunga chuoni hapo.

Ameongeza kuwa mwaka 2027 Tanzania itakuwa na Kongamano kubwa la wafugaji nyuki la ' Apimondia' hivyo wao kama wahitimu waanze kubuni kupitia taaluma walizopata namna ya kutengeneza kipato kupitia Kongamano hilo.

Aidha, Katika kuhakikisha chuo hicho kinapiga hatua Dkt. Kohi amesema serikali ipo mbioni kuboresha karakana  zilizopo chuoni hapo ili ziwe na vifaa vya kisasa ambavyo wanafunzi watakao kuwa wakisoma chuoni hapo waweze kupata elimu bora na ya kisasa Zaidi.

Vilevile, alitumia fursa hiyo kuwahidi kuwa Wizara itashirikiana na wadau wengine kuwatumia wahitimu hawa kadiri itakavyowezekana kwa kuwa chuo hicho ni cha kimkakati kwani lengo la Serikali ni kuona mazao mengi ya misitu yanazalishwa hapa nchini 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Bw. Deusdedith Bwoyo amesema anaamini Serikali pamoja na wadau mbalimbali watachukua fursa kuwaajiri wahitimu hao ili walete tija katika sekta ya misitu hapa nchini

Naye Mkuu wa Chuo cha Viwanda na Misitu Moshi (FITI), Dkt. Zakaria Lupala ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake kwa kuendelea na jitihada za kusaidia chuo hicho na kuwaomba waendelee kusaidia chuo hicho ili waendelee kutoa elimu bora kwa wanafunzi wanaojiunga chuoni hapo.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA