Akisoma risala ya shule kwenye mahafali hayo ,Mkuu wa shule ya Sekondari Little Treasures Alfred Mathias amesema wanafunzi hao walifundishwa na kuandaliwa vizuri katika taaluma ili waweze kukabiliana kikamilifu na mitihani ya taifa (NECTA) mwaka huu hivyo wanatarajia matokeo mazuri kwenye matokeo kama ilivyo kawaida ya shule hiyo.
“Tunapenda kuwafahamisha kuwa katika matokeo ya mitihani ya mock shule yetu ilikuwa ya pili mkoa kati ya shule 154 na ya kwanza kwenye wilaya kati ya shule 26 kwa kufanya vizuri kwa kupata wastani wa daraja ‘A’, hii ni ishara nzuri kwa mitihani yao ya taifa ambayo wameifanya kutoka tarehe 13 hadi 24/11/2013”, amesema Alfred Mathias.
Alfred Mathias
“Pia tunayo furaha kuwaarifu wazazi na walezi juu ya matokeo mazuri ya shule ya msingi Little Treasures katika mitihani ya kumaliza darasa la saba 2023 tumefaulu kwa wastani wa alama 46 ya 50 wanafunzi wote wameweza kupata wastani wa ‘A’ na kufanikiwa kuwa wa kwanza kwenye wilaya kati ya shule 56 na wa kwanza kwenye mkoa kati ya shule 658 katika kundi letu matokeo haya mazuri ni kwa ushirikiano mzuri kati yetu na wazazi/walezi kwa ushauri, michango na ada wanazotoa tunashukuru kwa ushirikiano wanaotupatia”, amesema Alfred Mathias.
"Kutokana na maendeleo ya teknolojia shule imefanikiwa kufundisha masomo ya Kompyuta ili kuwapa wanafunzi elimu na ujuzi wa kutumia kompyuta katika karne hii ya kidigitali lakini pia tunaushukuru viongozi wa elimu mkoa, wilaya na kata kwa ushauri na maelekezo yao katika masuala ya kitaaluma kulingana na miongozo ya serikali”, ameongeza Alfred Mathias.
Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Meneja wa shule za Little Treasures Wilfred Mwita amesema shule za Msingi na Sekondari Little Treasures zimekuwa chachu kubwa katika sekta ya elimu katika mkoa wa Shinyanga na taifa kwa ujumla huku akiahidi kuwa wataendelea kuboresha zaidi miundombinu ili kuwawezesha shule wanafunzi kupata elimu yenye ubora na uhakika.
Wilfred Mwita
“Tunawashukuru wazazi na walezi kwa kuendelea kutuamini sisi Little Treasures kuwa sehemu sahihi ya kupata elimu yenye viwango bora, elimu tunayoitoa imekuwa chachu kubwa katika sekta ya elimu ndani ya mkoa na taifa kwa ujumla”, amesema Wilfred Mwita.
Lucy Mwita
Mkurugenzi wa Shule za Msingi na Sekondari Little Treasures, Lucy Mwita amesema tangu shule ya sekondari Little Treasures ilipoanzishwa imeendelea kufanya vizuri kwenye mitihani ya taifa na imekuwa ikipata wanafunzi katika uwiano sawa kati ya wasichana na wavulana na kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu na kuahidi kuja na mpango wa kuanzisha utoaji elimu ngazi ya juu ambayo ni kidato cha 5 na 6 kwenye shule hiyo.
Naye Mgeni Rasmi Kaimu Meneja kutoka Benki ya NMB Shinyanga Erick Marandu kwa niaba ya meneja wa benki hiyo ameipongeza shule ya sekondari Little Treasures kwa maendeleo mazuri katika elimu na kuupa heshima mkoa huo kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa huku akiwasihi wanafunzi hao waliohitimu kidato cha nne kutojihusisha na makundi yasiyofaa mara baada ya kuhitimu masomo yao na kutoshiriki vitendo viovu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na uasherati.
Erick Marandu
إرسال تعليق