Ni mamia ya waombolezaji wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Hai Mhew. Saashisha Mafuwe wameshiriki katika ibada ya maziko ya aliyekuwa katibu wake na Mwalimu mstaafu Benson Lema aliyeaga dunia mnamo Januari 2, 2024 katika hospitali ya Machame huku wakimzungumzia kama mpenda maendeleo na mtu aliyejitoa katika jamii.
Ibada hiyo ya maziko imefanyika leo Januari 7, 2024 katika Usharika wa Nronga Machame ambapo Mbunge Mhe. Saashisha Mafuwe alipata wasaa wa kuzungumza wakati wa zoezi la kuuaga mwili wa marehemu na kusema kuwa Mwl. Benson Lema enzi za uhai wake alikuwa kiungo mkubwa katika jamii na moja ya mtu aliyependa kujishusha kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kila nafasi aliyotumika huku akimwelezea kama nguzo ya mtu aliyesimama katika mstari bora wa maadili na uongozi.
Mhe. Saashisha amesema kuwa maisha ya Mwalimu Benson Lema yamefanyika baraka kwa jamii yake na kwamba ni wazee wachache wanaopenda jamii yao kwa dhati kwani katibu huyo alikuwa mwadilifu wa kweli na mtu asiyependa mzaa hasa katika utendaji wake wa kazi.
Katika ibada hiyo pia Mchungaji Calvin Kessy wa usharika wa Uswaa aliyemwakilisha Mkuu wa Jimbo la Hai amesema kuwa Mwalimu Benson Lema aliishi maisha yenye maadili ambapo vijana wengi wa sasa wanashindwa kuyaishi hasa pale wanapoishi maisha ya kubweteka na kuwa tegemezi kwa wazazi wao.
Kwa upande wao baadhi ya waombolezaji waliotoa salamu za rambirambi wamemzungumzia mwalimu Benson Lema kama mmoja wa mtu aliyependa kutengeneza viongozi katika jamii huku akijitoa katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Hai Katibu tawala wa Wilaya ya Hai Sospeter Magonera amesema kuwa wilaya imepoteza mchapa kazi na mpenda maendeleo na kwamba alikuwa na busara na hekima na msaada kwa watu wengi.
Mwalimu Benson Lema alistaafu rasmi kazi ya ualimu mwaka 2014 na kisha mwaka 2020 Mbunge Saashisha Mafuwe alimuomba awe katibu wake, kazi aliyoifanya hadi umauti ulipomfika.
BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.
إرسال تعليق