SERENGETI BYTES YAZINDUA ORODHA YA WANAMABADILIKO 100 WA TANZANIA MWAKA 2023

 

Katika juhudi za kutambua mafanikio na matokeo chanya yanayotokea Tanzania kama sehemu ya kutengeneza historia nzuri ya nchi, Serengeti Bytes imezindua Orodha ya Wanamabadiliko 100 wa Tanzania ya mwaka 2023.

 Orodha hiyo iliyoandaliwa na kampuni hiyo ya mawasiliano, masoko, na teknolojia inaangazia juhudi za kipekee za Watanzania walio mstari wa mbele kuleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. 

Kennedy Mmari, Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Bytes ambaye pia ni mhariri wa orodha hiyo, ameweka msisitizo wa umuhumimu wa kutambua mabadiliko chanya katika jamii na taifa na watu walio nyuma ya michakato ya mabadiliko hayo. "Orodha hii ya wanamabadiliko inalenga kuwatambua Watanzania wanaojitolea kuleta mabadiliko chanya na kuonyesha namna ambavyo kuanzia raia wa kawaida mpaka wale walio na nyadhifa wanaweza kutumia nguvu walizonazo kubadilisha jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla," amesema Mmari.


Mmari ametanabaisha kwamba uvumbuzi ambao ni injini katika safari ya kila mwanamabadiliko umezingatiwa kama kigezo muhimu katika kuandaa orodha hiyo ya Wanamabadiliko 100. "Uwezo wa kufikiri tofauti na kutafuta suluhu bunifu kwa matatizo magumu unawatofautisha wanamabadiliko hawa. Orodha hii imebeba mawazo na miradi ya kibunifu inayowahamasisha wengine kuwa wavumbuzi katika kujikwamua kimaisha na kuchangia mabadiliko ya jamii na taifa," amefafanua Mmari. 


Michael Mallya, Afisa Uendeshaji wa Serengeti Bytes ambaye ni mhariri wa orodha hiyo, amezungumzia kwa undani mambo yaliyomo kwenye orodha hiyo na jinsi ambavyo orodha hiyo imegusa sekta tofauti zinazochochea maendeleo katika ngazi ya jamii na taifa kwa ujumla. “Kuanzia wajasiriamali jamii wanaoleta mapinduzi makubwa kwenye elimu mpaka wanaharakati wa mazingira wanaotetea uendelevu, kila hadithi ni ushahidi wa nguvu ya uthubutu na ustahimilivu katika kuleta mabadiliko. Hawa ni watu waliochagua kupambana na kuleta mabadiliko ya kudumu,” amesema Mallya. 


Mallya ameongeza kwamba lengo la kuandaa orodha hiyo ni kuchochea ushirikiano baina ya sekta na baina ya wanamabadiliko hao kwa kutambua kwamba mabadiliko ya msingi na yenye uendelevu mara nyingi yanahitaji juhudi za pamoja. Mallya alisema, "Orodha hii inahimiza ushirikiano wa kisekta na kitaaluma kwa kuonesha matokeo chanya kwenye sekta mbalimbali na watu wanaowezesha mabadiliko hayo. Kwa kufanya hivyo tunatarajia wanamabadiliko hao wataungana na kubadilishana maarifa na uzoefu sambamba na kufanya kazi kwa pamoja katika kujenga maisha bora ya baadae," ameongeza.


Orodha hii ya Wanamabadiliko 100 ni uthibitisho wa uwepo wa watu wenye uthubutu na kujitoa kwa kiwango cha juu ili kuleta mabadiliko chanya. Orodha hii inasheherekea hatua za kujenga Tanzania bora bila kujali ukubwa wa mabadiliko. "Kupitia matendo yao, wanamabadiliko hawa wanatutia moyo sisi sote kuchukua hatua kuleta mabadiliko, na kuwa sehemu ya mabadiliko tunayotamani kuyaona duniani," amehitimisha Mallya.

Orodha hii inapozinduliwa, wito unatolewa kuungana katika kusherehekea watanzania hawa wanaochukua hatua za kipekee. Tunapaswa kuendelea kutambua safari zao, kukuza sauti zao kwa pamoja, kusherehekea mafanikio yao, na kuamsha vuguvugu la mabadiliko linaloacha urithi wa kudumu kwa vizazi vijavyo.

Orodha kamili inapatikana kwenye tovuti ya Serengeti Bytes kupitia kupitia https://rb.gy/3wa1ut

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA