Na Mwandishi wetu- Dodoma
Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imesema imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 kilogramu zaidi ya milioni moja za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari tarehe 20 Februari 2024 Jijini Dodoma kuhusu taarifa ya mafanikio ya Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Mhe. Jenista alisema Watuhumiwa 10,522 walikamatwa ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wanawake ni 821 huku akisema kuwa jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa.
“Kiasi cha dawa zilizokamatwa kwa mwaka mmoja ni zaidi ya mara tatu ya dawa za kulevya zilizokamatwa kwa kipindi cha miaka 11 hapa nchini, kwani miaka 11 iliyopita tulifanikiwa kukamata kilogramu 660,465 pekee. Aidha, Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria,” Alisema Mhe. Jenista.
Waziri Jenista amesema mafanikio ya ukamataji huu yanatokana na nia, utashi na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan. “Mara baada ya kuingia madarakani ameonesha dhamira yake kwa vitendo katika kuiimarisha Mamlaka kwa kuipa vitendea kazi vinavyohusianisha teknolojia ya kisasa ya kimkakati katika mapambano, kutoa mafunzo kwa watumishi ndani na nje ya nchi pamoja na uzalendo wa watendaji kwenye Mamlaka”.
Pia aliongeza kwamba Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa lengo la kutoa elimu ya dawa za kulevya na rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa nchini ambapo sasa zitaitwa klabu za kupinga rushwa na dawa za kulevya.
“Tafiti zinaonesha kwamba, matumizi ya dawa yanaanza katika umri mdogo kati ya miaka 10 na 12 hivyo Serikali imeona iweke mkazo huko kwani watoto wengi wanapitia katika shule hizo na elimu imeendelea kutolewa katika makundi ya kijamii yakiwemo ya viongozi wa dini, viongozi wa kimila, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama, maafisa forodha na wakulima hasa katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha bangi na mirungi,”Alieleza.
Aidha alifafanua kwamba Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa kuongeza vituo vya kutolea tiba kwa waraibu kwa kutumia dawa na huduma za unasihi (MAT) ambapo kwa mwaka 2023 kituo kimoja kilifunguliwa mkoani Morogoro katika gereza la kihonda ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2023, jumla ya vituo 16 vilikuwa vinatoa huduma kwa walengwa.
“Vituo vingine viwili katika wilaya ya Muheza – Tanga na Chalinze - Pwani vinatarajia kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2024. Vituo vingine vitatu vitaanza kujengwa katika mikoa ya Shinyanga, Kilimanjaro na Pwani (Mkuranga). Aidha, serikali iko kwenye hatua za mwisho za ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za Tiba na utengamao (Rehabilitation centre) katika jiji la Dodoma,”Alibainisha Mhe. Jenista.
Kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Nchi zingine alisema kuwa Tanzania imekuwa ikishirikiana na nchi mbalimbali kikanda na kimataifa katika kupambana na dawa za kulevya ambao unahusisha kubadilishana taarifa za kiusalama kuhusu dawa kulevya, na kujengeana uwezo katika mapambano hayo.
“Hivi karibuni tumesaini hati ya makubaliano kati ya Tanzania na Zambia kushirikiana kudhibiti biashara ya dawa za kulevya. Baadhi ya faida zilizotokana na ushirikiano huu ni kufanikisha ukamataji wa baadhi ya watuhumiwa wanaohusishwa na kilo 3,522. 52 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine zilizokamatwa mwezi Disemba, 2023 pamoja na ukamataji wa kilo 423.54 za skanka ulitokana na ushirikiano mzuri kati yetu na Zambia,”Alifafanua.
Aidha alihitimisha kwa kueleza kuwa Serikali itaendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hususani katika uboreshaji wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza kasi ya mapambano na hatimaye kumaliza tatizo la dawa za kulevya nchini.
إرسال تعليق