VIONGOZI WANAWAKE WAFUNDWA NAMNA YA KUKABILIANA NA MASHAMBULIZI MTANDAONI

Mratibu wa Mradi POLLICY Najma Matengo akizungumza 


Na Rose Ngunangwa - Dar es salaam

Viongozi wanawake wameaswa kutoa ufafanuzi pale kunapokuwa na habari za uzushi dhidi yao na kukwepa kujibu mashambulizi pale wanaposhambuliwa mtandaoni kwani kufanya hivyo kutawafanya kupoteza dira.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Najma Matengo Mratibu wa Mradi kutoka POLLICY wakati wa kikao kazi na madiwani wanawake na waandishi wa habari chini ya mradi wa VOTE: WOMEN.

Akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya teknolojia ya kidijiti na habari, Matengo alisisitiza umuhimu wa kutoa ufafanuzi pale mtu anaposhambuliwa au kusambaziwa taarifa za uzushi badala ya kujibu mashambulizi kwani kutotoa ufafanuzi kutaifanya jamii kuamini taarifa hizo.


“Viongozi wanawake wanatakiwa kujua muktadha wa utamaduni na aina gani ya maudhui ya kuposti ikiwemo kuangalia muonekano wao kimavazi. Ni vema akaunti za kazi zikaweka picha zinazoendana na maudhui na sio selfie,” alisema.

Akisimulia moja ya changamoto alizopitia kama mgombea mwanamke, Lucy Lugome Diwani kutoka Segerea alisema katika moja ya chaguzi alishambuliwa na mmoja wa wagombea kutoka chama pinzani ambapo alizusha kuwa yeye alikuwa mwanamke asiye na maadili wala familia.

“ Ili kukabiliana na tuhuma za kwamba mimi ni mwanamke nisiye na maadili nilimwomba Mume wangu na watoto kuambatana nami ambapo alisimama na kuninadi katika kampeni na nikashinda,” alisimulia.

Kwa upande wake, Beatrice Nyamisango ambaye ni mheshimiwa Diwani wa Jiji la Dar amesisitiza umuhimu wa kutumia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii ili jamii iweze kujua wao ni nani.

“ Sisi kama wanawake viongozi ni lazima tuendelee kujenga mahusiano mazuri na vyombo vya habari ili kazi zetu zitambulike,” alisema Nyamisango.

Katika kikao kazi hicho madiwani wanawake walifundishwa pia namna ya kutengeneza akaunti za Linkedln na kuelekezwa aina ya maudhui ya kuweka.

Shirika la POLLICY ni kikundi cha teknolojia ya kiraia cha wanawake wa Afrika Mashariki ambapo kazi na tafiti zao zinahusisha matumizi ya utekelezaji wa taarifa na teknolojia ili kuunda mabadiliko ya kijamii.

Kikao kazi hiki kinakuja huku Tanzania ikijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA