RC MTAMBI ATOA MAAGIZO KWA WAKUU WA WILAYA, WAKURUGENZI NA VYAMA VYA USHIRIKA MKOA WA MARA

             


           

 Na, Ernest makanya - Fichuzinewsblog, Musoma.


Mkuu wa Mkoa wa Mara  Kanali Evans Mtambi  amevitaka vyama vya ushirika kusimamia vizuri vyama na kuhakikisha vinapanua wigo wa uzalishaji wa mazao yenye tija kwa wakulima.


Ametoa maelekezo hayo wakati akihutubia mkutano wa siku mbili wa Jukwaa la Maendeleo ya Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mara, ulioanza leo Jumatano katika ukumbi wa CCM mjini Musoma.


Amevikumbusha vyama vikuu vya ushirika WAMACU Ltd na PMCU kusimamia vizuri vyama vya msingi na kuhakikisha vinaongeza uzalishaji wenye tija katika mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa na pamba.


Pia Rc Mtambi amevitaka vyama hivyo kuhakikisha kuwa madeni vilivyokabidhiwa na iliyokuwa MCU Ltd yanalipwa kwa wakati. “Kwa kufanya hivyo kutajenga na kuimarisha taswira ya ushirika wa kibiashara kwa manufaa ya kiuchumi kwa jamii yetu,” Amesema Mkuu wa Mkoa huo.


Sambamba na hilo, amewataka viongozi wa vyama hivyo kusimamia kikamilifu mali za ushirika, kufanya vikao na kusoma taarifa kwa wanachama kwa uwazi.


Kuhusu msimu wa ununuzi wa pamba uliozinduliwa kitaifa Mei 8, mwaka huu, RC Mtambi amewaelekeza viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) kusimamia vizuri shughuli hizo na kuhakikisha wakulima wanapata stahiki zao.


Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa maagizo kwa Maafisa ushirika kufuatilia ununuzi wa zao la Pamba ikiwa ni pamoja na kutoa maagizo kwa wakuu wa Wilaya na wakurugenzi Mkoani humo kutatua migogoro ya ardhi kati ya vyama vya ushirika, taasisi za umma na watu binafsi.

“Maafisa ushirika wafuatilie kwa karibu ununuzi wa pamba na kutoa taarifa kwa wakuu wa Wilaya endapo wataona kuna mwenendo usiofaa, ikiwa ni pamoja na changamoto ya wakala wa upimaji, Miogoro hii imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya sekta ya ushirika… nawaelekeza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kukaa na wanaushirika na kupitia changamoto hii, kisha kwa pamoja kutafuta nama ya kuikabili,” amesema.


Hata hivyo amehitimisha kwa kuwataka wanaushirika kila mmoja kwa nafasi yake kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu.



Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA