Zuhura Yunus
Juni 8, 2024
Na Mwandishi Wetu
Mwezi Februari 2022, Zuhura Yunus alianza kazi rasmi kama Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.
Zuhura alipata uteuzi huo akitokea Shirika la Habari la Uingereza (BBC) jijini London, ambako alifanya kazi kwa karibu miaka 15.
Mtaalamu huyo wa mawasiliano wa kimataifa ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili (Masters) kwenye mawasiliano ya umma kutoka Chuo Kikuu cha Leicester cha Uingereza.
Ifuatayo ni orodha ya mambo makubwa 10 aliyofanya akiwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais katika muda aliohudumu kwenye nafasi hiyo wa miwili na nusu:
1. Mahojiano ya Rais na vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa
Aliandaa mahojiano ya Rais Samia na vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa, ikiwemo Bloomberg, BBC, DW, Forbes, New York Times, Economic Times of India, Essence magazine (Marekani) na Paris le Monde (Ufaransa). Hii ni baada ya Rais wa Tanzania kukaa muda mrefu bila kuwa na mahojiano na vyombo vya habari vya kimataifa. Pia alisimamia mahojiano ya Rais na vyombo vya habari vya ndani, ikiwemo Azam, TBC na Mwananchi Communications.
2. Utoaji wa Taarifa kwa Umma (Press Release) za lugha mbili za Kiingereza na Kiswahili
Zuhura alikuta Taarifa kwa Umma (Press Release) za Rais zote zinatolewa kwa lugha moja tu ya Kiswahili. Kutokana na uzoefu wake wa kimataifa, alianza kutoa baadhi ya taarifa muhimu za Rais kwa lugha zote mbili za Kiingereza na Kiswahili kwa ufasaha mkubwa ili kufikisha taarifa za Rais kwa jumuiya ya kimataifa, wawekezaji wa nje na watalii.
3. Ubunifu wa Songa na Samia
Zuhura alibuni na kuanzisha kipindi cha televisheni cha kila mwezi cha Songa na Samia na kukitengeneza kwa weledi kuelezea mafanikio ya Serikali ya Rais Samia kwa kutumia takwimu na maelezo yenye ushawishi mkubwa. Kipindi chake cha Songa na Samia kilirushwa na televisheni zote kubwa nchini pamoja na TV za kwenye YouTube. Pia alibuni video fupi fupi za Songa na Samia na mabango (infographics) yaliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo WhatsApp, Twitter (X), Instagram na Facebook.
4. Kusafiri na waandishi kwenye ziara za Rais nje ya nchi
Zuhura alikuta waandishi wa habari nchini hawasafiri na Rais Samia kwenye ziara zake nje ya nchi. Akaanzisha utaratibu wa kusafiri na waandishi wa habari na wahariri kwenye ziara za Rais Samia nje ya nchi ili waandishi wapate uzoefu zaidi na ziara za Rais zitangazwe kwenye vyombo vya habari.
5. Mikutano na Waandishi wa Habari Ikulu
Zuhura alianzisha mikutano na waandishi wa habari (Press Conference) Ikulu, ambapo aliwaalika mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa taasisi mbalimbali kukutana na waandishi wa habari na wahariri kuzungumzia masuala mazito ya kitaifa, ikiwemo tume ya haki jinai na mafanikio ya ziara za Rais nje ya nchi.
6. Mawasiliano ya Rais Kidijitali
Zuhura alisimamia uanzishaji wa akaunti za Mawasiliano ya Rais kwenye mitandao mingi zaidi ya kijamii, ikiwemo Spotify, Podcast, TikTok ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa taarifa za Rais kwa wananchi.
7. Mawasiliano ya Rais ya Kimkakati
Zuhura alileta weledi kwenye mawasiliano ya Rais kwa umma kwa kulinda, kuimarisha na kuitetea taswira ya Rais. Alifanya kazi hiyo kwa umahiri mkubwa na kuepuka kuhusisha hadhi ya Rais na mijadala na vitu vilivyokuwa nje ya ofisi na hadhi ya Urais. Alifanya Mawasiliano ya Kimkakati kwa weledi mkubwa. Alihakikisha kuna upatikanaji wa taarifa za Rais kwa wakati na kufanya kazi za Rais na mafanikio yake yaonekana bayana (visibility).
8. Ubora wa video na picha
Tangu Zuhura aanze kufanya kazi Ikulu, ubora wa video na picha zinazotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais uliimarika na kuwa na viwango vya kimataifa.
9. Rafiki wa wanahabari
Zuhura amekuwa na urafiki wa karibu na wanahabari wa kimataifa na kitaifa. Amekuwa akikutana na waandishi wa habari ndani na nje ya Ikulu, pamoja na kushiriki kutoa msaada wa hali na mali kwa waandishi wa habari pale alipoweza. Amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwa wanahabari nchini katika kazi zao za kila siku.
10. Ngao ya Taswira ya Rais
Pengine kazi kubwa kuliko yote ambayo Zuhura aliyoifanya ni kuwa kama dodoki au ngao ya taswira ya Urais. Alitumia kufahamiana kwake na kuheshimika kwake na vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa kuimarisha taswira ya Rais kimataifa na kitaifa. Muda wote ambao Zuhura amekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, hakuna chombo cha habari chochote cha kimataifa au kitaifa (mainstream media) ambacho kimemshambulia moja kwa moja Rais na kuchafua taswira yake (direct attack on the Presidency).
إرسال تعليق