Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka viongozi kushirikiana na kuheshimiana ili kuchochea maendeleo ya watu na sio kukwamisha maendeleo
Dkt. Biteko amesema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Msangila, Kata ya Runzewe Magharibi, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Ameongeza kuwa maono ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwaona Watanzania wanapata maendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii nchini na ndiyo sababu ya kusukuma maendeleo kwa haraka katika kipindi chake cha uongozi ndani ya miaka mitatu ambapo amefanya kila kitu kwa viwango vya juu.
“Sisi wasaidizi wake anatuagiza wakati wote tukawasikilize wananchi kero zao, tusikilize shida zao na mimi nimekuja hapa kuwaambia Rais Samia anawapenda, anawathamini ataleta maendeleo zaidi,” ameongeza Dkt. Biteko.
“Mimi ni Waziri ninayeshughulika na Sekta ya Nishati, tulikua na shida ya umeme kwenye nchi yetu, umeme unakatika kwa sababu umeme mdogo mahitaji ni mengi, Mama Samia amesimamia, sasa hatuna mgawo wa umeme na tunaendelea kuimarisha miundombinu ya umeme,” amesisitiza Dkt. Biteko.
“Mnaona tunazungumza fedha kuja kujenga barabara, kujenga madarasa, tunazungumza hapa kukamilisha zahanati na tunazungumza hapa kuongeza visima vya maji, yote haya yanasukumwa na mpendwa wetu Rais Samia ili kutuletea maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Ameeleza kuwa, Rais Samia amefungua barabara katika wilaya ya Bukombe ikiwa na km 256 pekee, hadi sasa imeongezeka kufikia km 1400 na upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 20 tu lakini sasa kila sehemu wananchi wanapata huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella amewahimiza wananchi kuhakiki vitambulisho vya mpigakura ili kupata haki ya kuwachagua viongozi wanaowataka.
Naye, Diwani wa Kata ya Runzewe Magharibi, John Nguhi ameshukuru kwa fedha za maendeleo zilizotumika kuboresha huduma za Jamii na miundombinu ya Barabara.
إرسال تعليق