RC MTAMBI, WANAHABARI NA WADAU WA MAENDELEO WALIVYOBEBA MDAHALO WA MARA BORA KWA UWEKEZAJI NA KUISHI

 

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, viongozi wa MRPC na wadau mbalimbali wa maendeleo (wa nne kulia mbele) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhitimisha mdahalo huo. (Picha zote na Mara Online News)
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (katikati) akizungumza katika Mdahalo wa Mara Bora kwa Uwekezaji na Kuishi, mjini Musoma.  Wanaomsikiliza kwa makini ni Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob (wa pili kushoto), Katibu wa MRPC, Pendo Mwakyembe (kushoto), Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Mjanakheri Ibrahim (kulia) na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo sehemu ya Viwanda na Biashara, Gambaless Timotheo (wa pili kulia).
------------------------------------------------------

Na Christopher Gamaina, Musoma
----------------------------------------------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa maendeleo wamejadili fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo na kutaka msukumo wa kuzitangaza uongezwe ili zifahamike kwa watu wengi ndani na nje ya Tanzania.

Hatua hiyo ilifikiwa katika Mdahalo wa Mara Bora kwa Uwekezaji na Kuishi, ulioandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), na kufanyika kwenye Hoteli ya MK mjini Musoma jana

Fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Mara zilizotajwa na kujadiliwa katika mdahalo huo uliofana kwa aina yake, ni pamoja na ufugaji, uvuvi, uchimbaji madini, utalii na kilimo cha mazao ya biashara na chakula.
Sehemu ya waandishi wa habari walioshiriki mdahalo huo.
--------------------------------------------------

Katika hotuba yake, mgeni rasmi RC Mtambi alisema mkoa wa Mara una utajiri wa maliasili na rasilimali nyingi, lakini hazijatangazwa ipasavyo ili kuwashawishi watu wengi kujitokeza kuwekeza kwenye biashara zinazohusiana nazo.

Maliasili na rasilimali hizo ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti, Ziwa Victoria, madini aina ya dhahabu, mifugo na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara - kama vile mahindi, ndizi, kahawa, pamba, alizeti na viazi vitamu.

“Lakini pia, tuna miradi mikubwa iliyojengwa na inayoendelea kutekelezwa na serikali; tuna Uwanja wa Ndege Musoma, Hospitali ya Rufaa Kwangwa, Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere kule Butiama, na barabara zinaendelea kuboreshwa katika mkoa mzima.

“Neema hii tuliyo nayo katika mkoa wa Mara haijatangazwa vizuri. Ninawaomba waandishi wa habari mtumie kalamu zenu kutangaza fursa hizi kwa maendeleo ya mkoa wetu na Taifa kwa ujumla,” alisema RC Mtambi.

Kiongozi huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo pia kuipongeza MRPC kwa kuandaa mdahalo huo na kuanzisha mpango wa tuzo za kila mwaka kwa waandishi wa habari wa mkoani Mara watakaokuwa wanafanya vizuri.
Waandishi wa habari wakifuatilia mada katika mdahalo huo.
-----------------------------------------------

Awali, Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob alimshukuru RC Mtambi kwa kukubali kuwa mgeni rasmi, pamoja na wadau wa maendeleo walioitikia wito wa kushiriki mdahalo huo.


Tuzo kwa waandishi

Kuhusu tuzo kwa waandishi wa habari - zitakazojulikana kwa jina la Mara Quality Journalism Awards, Jacob alisema zitaanza kutolewa Desemba mwaka huu na kwamba washindi watazawadiwa vyeti na fedha taslimu.

“Tuzo hizi zitakuwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha uandishi bora (promoting quality journalism), ambao pia unachangia kuufanya mkoa wa Mara kuwa sehemu bora kwa uwekezaji na kuishi.


Alitaja makundi ya habari zitakazohusika katika tuzo hizo kuwa ni kilimo, ufugaji, madini, utalii, ujenzi na miundombinu, uhifadhi wa wanyamapori, maji, uvuvi endelevelu (sustainable fishing) na makundi maalum ya jamii.


“Tunaamini uandishi bora, yaani quality journalism katika maeneo hayo utasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongoza na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuharakisha maendeleo ya mkoa wa Mara na Taifa letu la Tanzania kwa ujumla,” alisema Jacob.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa MRPC (kushoto) alimkabidhi RC Mtambi zawadi ya kumkaribisha mkoani Mara, yenye picha yake na fursa za uwekezaji zinazopatikana mkoani humo, iliyoandaliwa na klabu hiyo.


Mbali na waandishi wa habari, baadhi ya wadau wa maendeleo wa mkoani Mara walioshiriki katika mdahalo huo ni kutoka Mgodi wa Barrick North Mara, Grumeti Reserves/ Grumeti Fund, HAIPPA PLC, Nyihita Sunflower, CCM, TANROADS, TCCIA, WAMACU, Kampuni ya Swala na Benki ya Azania, miongoni mwa wengine.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA