TPDC KUANZA UZALISHAJI WA GESI ASILIA, VISIMA VYA GESI NTORYA

Muonekano wa Kisima cha gesi asilia Ntorya-2 kilichopo katika kata ya Nanguruwe, mkoani Mtwara
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na kampuni ya mafuta ya ARA lipo mbioni kuanza uzalishaji wa gesi asilia katika visima vya gesi vya Ntorya 1 na Ntorya 2 vilivyopo mkoani Mtwara kata ya Nanguruwe katika kijiji cha Namayhakata Shuleni barabarani. Hatua hii inafikiwa ikiwa ni zao la juhudi zinazofanywa na TPDC kwenye shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara , Kijiji cha Nanguruwe

Katika kuelekea hatua ya kuvuna gesi hiyo TPDC imejikita kwenye kutoa elimu ya mradi kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuelimisha viongozi wa serikali kwa ngazi zote za mkoa na wilaya pamoja na kufanya mikutano ya hadhara na wananchi watakao guswa na mradi huo. Kwa kuwa zoezi la uendelezaji linahitaji ardhi kwa ajili ya ujenzi wa mitambo na miundombinu mingine TPDC/ARA wanashirikiana na kampuni mshauri mwelekezi kwenye masuala ya  uthamini APY-KEGS ili kuhakikisha masuala yote ya utwaaji wa ardhi yanafanyika kwa ustadi.

Akiongea katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Julai 6, 2024 katika kijiji cha Nanguruwe Meneja mradi wa Ntorya Patrick Kabwe alisema kuwa:-

"Shughuli za uzalishaji kwa visima hivi viwili vya gesi zinatarajiwa kuanza mwezi Aprili, 2025 ambapo kila kisima kitakuwa na auwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 20 kwa siku , pia tunategema kuchimba kisima cha tatu kinachoitwa Chikumbi-1 ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 20. Kwa awamu ya kwanza kwa visima vyote vitatu kutakuwa na uzalishaji wa jumla ya futi za ujazo milioni 60 kwa siku".

"Aidha, awamu ya pili ya uzalishaji TPDC itachimba visima vinne katika kata ya Nanguruwe ambapo uzalishaji utafikia futi za ujazo milioni 140 kwa siku", alisema Kabwe.
Meneja mradi wa Ntorya Patrick Kabwe akielezea mradi kwa wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Nanguruwe.

Katika hatua nyingine Kabwe alishukuru uongozi wa mkoa na wilaya kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha mradi huu.

"Sisi TPDC pamoja na ARA Petroleum tunashukuru serikali ya Mkoa na Wilaya kwa ushirikiano wanaotupatia kwani bila wao tusingekuwa tumefika hapa, ushirikiano wanaotupatia ndio unasaidia mpaka sasa mradi unaendelea",aliongeza.

Naye Mwakilishi wa kampuni ya ARA Judith Kalugasha alisema kuwa "Mradi huu wa gesi sio wa kwanza kwa kata ya Nanguruwe, kinachoifanyika hapa hususani kwenye uthamini wa ardhi ni muendelezo tu wa miradi mingine iliyopoita hivyo tunategemea ushirikiano kutoka kwa wanachi ili mradi huu ukamilike kwa wakati"
Mwakilishi wa Kampuni ya ARA-Judith Kalugasha akitoa ufafanuzi wa jambo katika mkutano wa hadhara –Nanguruwe

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa TPDC Bw. Oscar Mwakasege alieleza umuhimu wa miradi ya gesi asilia kwa jamii ikiwa ni pamoja na ajira, uboreshwaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama afya, elimu , maji na utawala bora.

"TPDC tunafanya kazi na jamii hivyo tunawajibika katika kuleta ustawi wa huduma za kijamii kwenye vijiji ambavyo tunatekeleza miradi ya gesi asilia ikiwemo kijiji cha Nanguruwe",alisema.


Vilevile, Diwani wa kata ya Nanguruwe Mhe. Patrick Simwinga alipongeza TPDC na Kampuni ya ARA Petroleum kwa kuwa na mpango mzuri wa kushirikisha jamii katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutekeleza mradi huo.

TPDCTUNAWEZESHA


Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA