UCHUMI WA BULUU NI SHUGHULI ZOTE ZA KIUCHUMI ZINAZOHUSIANA NA BAHARI, MAZIWA MAKUU NA RASIRIMALI ZAKE - DKT. BITEKO

Na, Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kulinda viumbe vya baharini na kuhifadhi mazingira ya bahari kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo.


Dkt. Biteko amesema hayo leo Julai 4, 2024 wakati akifungua kongamano la Tatu la Uchumi wa Buluu mwaka 2024 yenye kaulimbiu: Kuunganisha Usalama Baharini, Utunzaji wa Mazingira na Maendeleo ya Teknolojia kwa ajili ya Ukuzaji wa Uchumi wa Buluu


“Tunapofanya majadiliano leo, tujikite kwenye kanuni uendelevu, usawa na uvumbuzi ili hatimaye kongamano hili liwe mwanga unaotuongoza kwenye uchumi wa buluu unaoinua jamii zetu, ninawasihi kila mmoja wenu ashiriki kikamilifu ili tuweze kupata matokeo chanya ya kongamano hili,” amesema Dkt. Biteko.


Amesema uchumi wa buluu unatambuliwa kama mchangiaji mkubwa wa maendeleo endelevu ambapo jamii hutumia rasilimali za bahari kwa njia ambayo ni endelevu na kwa kiasi kikubwa huzingatia uhifadhi wa mazingira.


Pia, uchumi wa buluu huchochea uvumbuzi wa fursa kama vile teknolojia ya kibayoteknolojia na nishati ya bahari, kutoa suluhu za nishati mbadala na tiba, inasaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia ulinzi wa mifumo ikolojia, na kuhakikisha Ulinzi na usalama wa bahari, ambao ni muhimu kwa usalama wa usafiri wa majini na kuzuia shughuli haramu baharini.


“Pamoja na mazuri yote hayo, uchumi wa buluu unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya hali ya hewa, uvuvi haramu, uharibifu wa makazi na kutopatikana kwa taarifa sahihi. Kama ilivyo katika nchi nyingine duniani, Tanzania pia inakabiliwa na changamoto hizo,” amesisitiza Dkt. Biteko.


Dkt. Biteko ameongeza kuwa, mwaka 1991 Tanzania ilianzisha Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ambapo majukumu yake ni pamoja na kushirikiana na vyuo vingine katika kufanya tafiti, kubadilishana wataalam na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali, watu binafsi na wadau wengine kuhusiana na maswala ya bahari.


“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ibara ya 136 (e) imeelekeza, kuibua na kuendeleza Sekta mpya za uchumi ikiwemo uchumi wa buluu (blue economy), ubunifu (creative industry) na uchumi wa kidigitali. Uchumi wa buluu ni shughuli zote za kiuchumi zinazohusiana bahari na maziwa makuu pamoja na rasilimali zake,” amesisitiza Dkt. Biteko.


Naye, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema uchumi wa buluu ni uchumi mtambuka unaohusisha sekta mbalimbali. Amesema kongamano hilo limekua chachu katika kutoa fursa na mafunzo kwa watanzania katika Sekta ya bahari.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema mkoa wa unahusika kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa buluu. Amewataka wadau kuendelea kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.



Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA