Imeelezwa kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba 2023 hadi Julai 2024 kiasi cha maombi 2648 ya utafutaji wa madini yamefutwa na kuondolewa kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 14 , 2024 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Bunge Nishati na Madini kuhusu hali ya Usimamizi na Uendelezaji wa Leseni zilizotolewa kwa ajili ya Utafutaji na Uchimbaji wa Madini.
Waziri Mavunde amesema kuwa maombi hayo yalifutwa baada ya kubainika kuwa, waombaji hawakuwa na nia ya kupatiwa leseni za utafutaji madini na badala yake walikuwa wameyashikilia na kuhodhi maeneo hayo na hivyo kuwanyima fursa wenye nia ya kuyaendeleza.
Waziri Mavunde amefafanua kuwa , Tume ya Madini inaandaa mwongozo na masharti ya namna bora ya kuomba maeneo hayo kwa wawekezaji wenye nia na uwezo wa kuwekeza kwenye Sekta ya Madini.
Waziri Mavunde ameongeza kuwa, Wizara kupitia Tume ya Madini imeendelea kutoa hati za makosa kwa wamiliki wa leseni kutokana na ukiukwaji wa masharti ya leseni zao kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123 ambapo jumla ya leseni 110 za utafutaji madini, leseni 13 za uchimbaji wa kati na leseni 2 za uyeyushaji wa madini zilipewa hati ya makosa.
Awali, akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Bunge Nishati na Madini, Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwambo amesema kwa kipindi cha Oktoba 2023 hadi Julai 2024 , Tume ya Madini ilitoa leseni moja ya uchimbaji mkubwa , leseni 20 za uchimbaji wa kati na leseni 7974 za uchimbaji mdogo katika maeneo mbalimbali nchini.
إرسال تعليق