Na John Bera - DODOMA
WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini imeanza kuandaa Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara utakaotumiwa kwa ajili ya shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini ya Sera, Mipango , Programu na Miradi inayotekelezwa na Idara, Vitengo na Taasisi za Wizara.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Kikao kazi cha Maafisa wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini na Maafisa Kiungo wa Idara na Vitengo wanaotekeleza majukumu ya Kitengo hicho, Bi. Bure Nassibu, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo hicho amesema Kitengo kina majukumu ambayo lengo lake ni kufanya ufuatiliaji na tathmini ya Sera, Mipango, Programu na Miradi iliyoko chini ya Wizara ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo, taratibu, muda, mipango na bajeti iliyopangwa.
"Kitengo kina majukumu 11, kwa sehemu kubwa ukiangalia kazi yetu kubwa ni kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Wizara ili kupima matokeo na ufanisi" amesema Bure.
Aidha, ameongeza kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa Kitengo hicho, maafisa hao watajengewa uwezo ili waweze kufanya kazi kwa weledi.
"Ili muweze kufanya kazi kwa ufanisi lazima mjengewe uwezo, hivyo tunaangalia namna ambavyo mnaweza kupata mafunzo ili muweze kufanya kazi kwa ufanisi" Amesema Bure.
Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini ni moja ya Kitengo muhimu katika Wizara na Serikali kwa ujumla kwani kazi ya Kitengo hicho ni kuhakikisha utendaji kazi ndani ya Wizara na Serikali kwa ujumla zinatekelezwa kwa ubora unaostahili.
إرسال تعليق