*Asema mradi huu una umuhimu wa kipekee
*Asema kiwanda hicho kinaenda kutoa uhakika wa sukari nchini, awapongeza NSSF na Jeshi la Magereza kwa kufanikisha mradi huo
Na MWANDISHI WETU, MOROGORO.
Historia imeandikwa na hakika hakuna kilichokwama! Unaweza kusema hivyo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzindua rasmi mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi, kilichopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro na kusema mradi huo anataka uwe endelevu kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Uzinduzi wa kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha sukari tani 50,000 kwa mwaka umefanyika tarehe 7 Agosti, 2024 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali. NSSF kupitia mradi huo imetekeleza moja ya jukumu lake la uwekezaji; majukumu mengine ni kuandikisha wanachama wapya kutoka sekta binafsi na sekta isiyo, kukusanya michango na kulipa mafao.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria hafla hiyo Mhe. Rais Dkt. Samia amewapongeza wana hisa wa kiwanda hicho ambao ni NSSF na Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali (SHIMA), kwa kukamilisha mradi huo wenye manufaa makubwa na kuwa Serikali inafanya kila jitihada kutanua mradi huo.
Aidha, amepongeza mradi huo kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania pamoja na wakulima kupata soko la uhakika wa kuuza miwa. Pamoja na hilo amepongeza mradi huo kutumia umeme ambao unaozalishwa kiwandani hapo. Amesema dhamira na malengo ya Serikali ni kuhakikisha mradi huo unakua na kuleta tija kubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema ujenzi wa kiwanda hicho unatokana na maono ya Rais Dkt. Samia ambaye aliahidi kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwemo wa Mkulazi. Amesema baada ya Rais Dkt. Samia kuingia madarakani mwezi Machi 2021, aliridhia mradi huo kuendelea na kuwa unaenda kupunguza nakisi ya sukari nchini na kutatua changamoto ya ajira.
Amesema uwekezaji wa mradi huo umeongeza wigo wa kodi na umechechemua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa ziara yake katika mkoa huo ambayo imekuwa na mafanikio makubwa hasa katika kuzindua miradi ya kimkakati ukiwemo wa kiwanda cha sukari Mkulazi ambao umetoa fursa nyingi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akitoa taarifa ya mradi wa kiwanda hicho, Dkt. Hildelitha Msita, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Mkulazi, amesema wataendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuondoa nakisi ya sukari nchini pamoja na kuongeza ajira kwa Watanzania kwa kusimamia uendeshaji wa kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka na tayari uzalishaji wa sukari ya majumbani ulianza tarehe 1 Julai, 2024 ambapo kwa siku kinazalisha tani 250.
Kwa upande wake Mhandisi Hamad Masauni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amesema mradi huo umekuwa na faida kwa Jeshi la Magereza na kuwa faida hizo zinatokana na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia kuhakikisha wanatumia vizuri rasilimali za Jeshi hilo kwa kuleta tija na kutoa mchango kwa jamii na Taifa.
Naye Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema uwepo wa mradi wa kiwanda hicho unatoa fursa mbalimbali kwa wananchi, hivyo watahakikisha kiwanda hicho kinazalisha sukari ya majumbani na viwandani na kinalindwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Aidha, Mhe. Dkt. Suleiman Jafo, Waziri wa Viwanda na Biashara, amesema Serikali ya awamu ya sita imeweka historia kubwa ikiwemo kuongeza idadi ya viwanda takribani 18,000 ndani ya miaka mitatu.
Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Profesa Kalamagamba Kabudi amesema wananchi wa jimbo hilo wanashukuru ujio wa kiwanda hicho ambacho kinawasaidia kupata ajira na kupata soko la uhakika la kuuza miwa yao.
إرسال تعليق