Zaidi ya Washiriki 280 kutoka Mabunge Wanachama wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CPA) Kanda ya Afrika watanaratajia kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 53 utakaofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 6, Oktoba Jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha, Katibu Msaidizi wa CPA Kanda ya Afrika, Ndugu Daniel Eliufoo alisema hadi sasa Mabunge 14 kati ya 19 yameshathibitisha kushiriki Mkutano huo ikewemo Bunge la Tanzania.
Aidha, alisema Maspika wa Mabunge ya Kitaifa waliothibitisha kushiriki Mkutano huo hadi sasa ni 10 na Manaibu Spika watatu pamoja na Manaibu Spika takribani 10 kutoka katika Mabunge ya Majimbo.
Alisema ufunguzi rasmi wa Mkutano huo utafanyika tarehe 3 Oktoba, 2024 na Mgeni Rasmi atakuwa ni Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ambaye atamuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alisema CPA Kanda ya Afrika imekuwa ikifanya mikutano yake mikuu ya kila mwaka kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali kwa kuzingatia malengo ya kuanzishwa kwa umoja huo.
“Lengo la kuanzishwa kwa Chama cha Mabunge ya Nchi za Jumuiya Madola ni kuchagiza amani, demokrasia, uwajibikaji na haki za binadamu miongoni mwa nchi wanachama.
“Mkutano huu wa CPA – Kanda ya Afrika ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha washiriki mbalimbali kwa lengo la kujadili masuala yanayowahusu kwa kuzingatia malengo ya kuanzishwa kwake .” alisema.
Alisema pamoja na mkutano mkuu wa mwaka, CPA imekuwa ikiandaa semina na mafunzo kwa lengo la kubadilishana uzoefu na pia imekuwa ikiandaa machapisho mbalimbali.
CPA ilianzishwa mwaka 1911 ikiwa na Kanda tisa ikiwemo Kanda ya Afrika ambayo ina wanachama 19 wa Mabunge ya Kitaifa na 64 wa Mabunge ya Majimbo.
إرسال تعليق