Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema ofisi yake inakaribisha washirika kusaidia katika nyanja mbalimbali zinazolenga kuboresha miundombinu ya elimu, mazingira ya kufundishi kwa walimu, usalama wa wanafunzi na kuongeza ufaulu wao.
Waziri Mchengerwa amesema Serikali pekee haiwezi kumaliza changamoto zote zinazoikabili sekta ya elimu na kusisitiza kuwa milango ya ushirikiano baina ya serikali na wadau wa maendeleo iko wazi ili kusaidia katika utatuzi wa changamoto unaolenga kuleta mabadiliko chanya.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo leo Septemba 05, 2024 ofisini kwake jijini Dodoma, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na mwenyekiti wa bodi ya mtandao wa elimu Tanzania Bi Faraja Kotta aliyeambatana na Mratibu wa kitaifa wa mtandao huo Bi Martha Makala.
Dhamira ya ujumbe huo kwa Waziri Mchengerwa ilikuwa ni kujitambulisha pamoja na kumshirikisha juu ya uwepo wa kongamano la kimataifa la ubora wa elimu litakalofanyika kuanzia Novemba 12 hadi 14 jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Waziri Mchengerwa amepongeza jitihada za mtandao huo za kuwakutanisha wadau wa elimu kutoka sehemu mbalimbali ili kujadali njia bora na endelevu za utatuzi wa baadhi ya changamoto katika sekta ya elimu na kusisitiza taasisi zingine zenye mlengo wa aina hiyo kuiga mfano huo.
Kwa mujibu wa Bi. Makala Kongamano hilo la nne la kimataifa la ubora wa elimu linatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 350 kutoka kwenye taasisi, asasi na mashirika zaidi ya 200 kutoka nchi 10 za Afrika.
إرسال تعليق