WAZIRI CHANA AKAGUA MIRADI YA KIMKAKATI HIFADHI YA TAIFA NYERERE

 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amekagua maboresho ya miradi mbalimbali ya kimkakati katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere Mkoani Ruvuma.

Akiwa katika ziara hiyo leo, Septemba 29, 2024 Mhe. Chana amekagua ujenzi wa kiwanja cha ndege, lango la kitalii la kisasa, nyumba ya wageni yenye vyumba nane na ujenzi wa nyumba za watumishi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa katika sekta ya Maliasili na Utalii ambapo alitoa fedha za UVIKO-19 zilizotumika kujenga miradi hiyo.

Ametoa maelekezo kwa TANAPA kuhakikisha lango la kitalii linaanza kutumika ili kuiingizia Serikali mapato huku akipongeza ubora wa nyumba za Askari Uhifadhi zilizojengwa katika eneo la Likuyu Sekamaganga.

"Tumepitia nyumba watakazokaa askari wa Jeshi la Uhifadhi zipo kwenye hali nzuri kabisa na nimeshatoa maelekezo geti lifanye kazi haraka kwa sababu limekamilika" Mhe. Chana amesisitiza.

Aidha, Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kuwaelekeza wawekezaji kukamilisha uwekezaji kwa wakati.

"Kuna watu wameshikilia maeneo katika maeneo yetu ya uhifadhi muda mrefu hakuna mtu anaendeleza, hii inaikosesha Serikali mapato na ajira kwa vijana " amesema Mhe. Chana.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya taifa Nyerere, Ephraim Anosisye Mwangomo amesema kuwa miradi hiyo ya “Gate Complex” na Uwanja wa ndege imegharimu takribani shilingi bilioni 2.1 kutokana na fedha za UVIKO-19.

Amesema hifadhi hiyo imeendelea kupata wageni wengi kutoka nje na kuongeza mapato yake hadi kufikia shilingi bilioni 11.9 kwa mwaka huu wa fedha ulioishia mwezi Juni 2024.

Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ni miongoni mwa hifadhi 21 zinazosimamiwa na Shirika Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na ina ukubwa wa kilomita za mraba 30,893 katika mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Lindi na Pwani.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA